Kwingineko

“Haiti imestahili Kufuzu Kombe la Dunia 2026” – kocha Migne

WILLEMSTAD: KOCHA wa timu ya taifa ya soka ya Haiti, Sebastien Migne, amesema kuwa umoja wa kikosi na ustahimilivu ndiyo ilikuwa siri kuu iliyopelekea taifa hilo kufuzu Kombe la Dunia la mwaka 2026, kufuatia ushindi wao wa magoli 2-0 dhidi ya Nicaragua.

Haiti ilishinda vikwazo vikubwa kufuzu kwa mara ya pili katika historia yao ya Kombe la Dunia, baada ya kushiriki kwa mara ya kwanza na matokeo mabaya mwaka 1974. Waliongoza kundi lao la kufuzu licha ya kukabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama.

Walilazimika kucheza mechi zao zote za kufuzu nje ya nchi yao, ambapo magenge yenye silaha yamechukua udhibiti wa karibu mji mkuu wa Port-au-Prince wote. Mgogoro huo umesababisha takriban watu milioni 1.3 kukimbia makazi yao na kuchochea hali ya njaa kali.

“Ni jambo la kufurahisha kwamba baada ya miaka 52 ya kukosekana, Haiti imefuzu kwa jukwaa hili kubwa zaidi la soka duniani,” Migne aliwaambia waandishi wa habari Jumanne nchini Curacao, ambako walicheza mechi yao ya mwisho ya nyumbani.

Migne alizungumza na mwandishi mmoja tu katika chumba cha mikutano kilicho wazi kabisa, tofauti kabisa na kumbi zilizojaa waandishi wa habari ambapo kwa kawaida makocha wa timu kubwa hukabiliana na maswali ya vyombo vya habari.

“Nina furaha kumfanya kila mtu ajivune wachezaji wangu, kwa sababu wanastahili. Wakati mwingine niliwasukuma wachezaji wakongwe kufikia mipaka yao, lakini haikuwa bure,” alisema Migne.

Haiti ilikuwa imeachwa nyuma katika msimamo wa kundi lao baada ya kupigwa mabao 3-0 na Honduras mwezi Oktoba, lakini walijikakamua na kuhakikisha wanamaliza kileleni mwa Kundi C kwa ushindi dhidi ya Costa Rica na Nicaragua katika mechi zao mbili za mwisho katika siku sita zilizopita.

“Hatukuwahi kupanic (kuingiwa na hofu). Najua jinsi ya kufanya hivyo kwa sababu nilifuzu Kombe la Dunia lililopita na nchi nyingine (kama kocha msaidizi wa Cameroon mwaka 2022). Ilikuwa ni kutulia, kufanya kazi kwa pamoja, na ndivyo tulivyofanya. Na zaidi ya yote, tulikuwa na ubora. Mara tu tulipoungana, sikuwa na shida.” – aliongeza meneja huyo.

Related Articles

Back to top button