AfricaAfrika Magharibi

GEORGE WEAH: Rais anayetarajiwa kuendeleza soka la Liberia

WAKATI mshindi wa zamani wa Ballon d’Or alipochaguliwa kuwa Rais wa nchi, Waliberia wengi walifi kiri kuwa bahati yao katika uwanja wa soka itabadilishwa.

Miaka minne na ushee sasa, wadau wa soka bado wana matumaini kuwa George Weah anaweza kuondoa au kubadilisha matatizo ya soka na kuusaidia mchezo huo wa kitaifa.

Weah mwenye miaka 55 aliapishwa kuwa Rais Januari 2018, akiahidi kubadilisha uchumi, kupambana na rushwa, kuboresha elimu, huduma ya afya na kutengeneza maelfu ya ajira kwa watu maskini.

Lakini wakati akielekea kukamilisha kipindi chake cha miaka sita ya uongozi katika Ikulu ya Liberia, baadhi ya mashabiki wake wakubwa wanaamini kuwa matatizo ya fedha katika soka na ukosefu wa maendeleo, miundombinu na uwekezaji katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi yenye uchumi ulioporomoka, bado ni kitendawili.

“Serikali ina vipaumbele vingine kama elimu, changamoto katika huduma za afya ni miongoni mwa mambo mengine muhimu,” anasema Mkurugenzi wa soka wa Chama cha Soka cha Liberia (LFA), Henry Browne.

“Katika miaka ya 1980 na ‘90, kila serikali iliingiza fedha katika soka, kitu ambacho hakifanyiki sasa. “Bado tuko nyuma kwa upande wa msaada wa fedha. Uzoefu ni mkubwa kwa serikali kutoka katika sekta zingine, lakini nafikiri inatakiwa kuongeza msaada wake ili tuanze kushindana.”

Wengi walitegemea Weah atakuwa Rais mwenye mafanikio katika soka kwa sababu alikuwa mwanasoka.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Liberia alitengeneza jina lake Ulaya katika klabu ya Monaco, Paris St-Germain (PSG) na AC Milan kabla hajacheza muda mfupi katika klabu ya Manchester City na Chelsea.

Wakati wa mkesha wa kuapishwa kwake kuwa Rais, wakati huo bosi wa LFA, Musa Bility alitabiri mwanga mzuri katika soka.

Baada ya yote, Weah aliahidi kufanya mabadiliko katika maisha ya Waliberia wote. Bility pia alikuwemo katika Kamati ya Utendaji ya Caf, Shirikisho la Soka Afrika, lakini alifungiwa kwa takribani miaka 10 na Fifa Julai mwaka 2019 baada ya kuvunja kanuni za soka.

CHANGAMOTO KATIKA SOKA

Liberia iliingia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe katika miaka ya 1990, lakini timu ya taifa ilikuwa na siku nzuri wakati huo, huku Weah akiongoza timu hiyo katika fainali ya Mataifa ya Afrika mwaka 1996 na 2002.

Akiwa bado mchezaji, alikuwa kama Mkurugenzi wa Ufundi wa timu hiyo kati ya mwaka 2000 na 2002 na mara kadhaa alikosa nafasi ya kuiongoza LFA baada ya kustaafu soka mwaka 2004, kabla mchezaji huyo hajabadili na kuelekea katika siasa mwa- ka mmoja baadaye.

Sasa SOKA ni miongo miwili tangu timu ya taifa ya Liberia ‘Lone Stars’ ishiriki katika mashindano makubwa na Uwanja wa Taifa wa nchi hiyo, Samuel Kanyon Doe (SKD) uwanja changamano, ulikuwa mmoja wa viwanja vilivyopigwa marufuku na Caf na Fifa kuendesha mechi hizo Agosti.

Liberia ina nafasi kubwa ya kuandaa fainali za Mataifa ya Afrika nchini Ivory Coast mwaka 2024, huku kundi lao la kufuzu likipunguzwa hadi kufikia timu tatu baada ya kujitoa kwa Zimbabwe.

Lakini mchezo wa ufunguzi kufungwa na Morocco, tatizo la fedha liliikumba LFA wakisaka kocha mpya baada ya kutoongeza mkataba na aliyekuwa kocha wao, Peter Butler.

Mchezaji wa zamani wa Lyon na PSG, James Debbah, ambaye pia ni binamu wa Weah, aliyeshirikiana naye kwa karibu miongo miwili, anaona siasa ni tofauti kabisa na soka.

“Tulifanikiwa wakati alipokuwa uwanjani,” alisema Debbah, mwenye umri wa miaka 52. “Kuna tofauti kubwa sana sasa kujaribu kumpatanisha kila mmoja, kuleta wachezaji wa kulipwa, kufanya kazi katika Wizara ya Vijana na Michezo na kujaribu kuirejesha nchi katika mstari wa soka.”

Alipoulizwa kama Weah alichukizwa na Liberia kushindwa kufuzu kwa mashin- dano makubwa tofauti na miaka ya nyuma, Debbah aliongeza: “Sifikiri kama inamkera. Amechangia makubwa katika soka katika nchi hii na bado anaendelea. “Kwa kweli huwezi kumlaumu kwa kile kinachotoka uwanjani kwa sasa. Yeye aliweka mazingira sawa kwa sisi kufuzu, lakini tumeshindwa.”

Kocha msaidizi wa Lone Stars, Thomas Kojo, mkurugenzi wa soka katika Wizara ya Vijana na Michezo, ambaye pia alicheza na Weah katika timu ya taifa ya Liberia, anasema: “Sisemi kuwa Rais achukue fedha zote kutoka serikalini na kuzipeleka katika soka, lakini kuna njia nyingi za kufanya ili fedha ziweze kuja katika programu za timu ya taifa.

“Kuna mambo tunaweza kufanya ambayo yatasaidia kuongeza fedha kwa sababu Rais hawezi kutumia kila fedha kuinua miundombinu ya soka. Kuna makampuni Liberia yanaweza kusaidia kujenga miundombinu ya soka. Kuna makampuni Liberia yanaweza kusaidia timu ya taifa…”

FEDHA ZA FIFA

Kama wanachama wengine wa Fifa, Liberia imefaidika na programu za maendeleo yaliyoanzishwa na shirikisho hilo la kimataifa la soka tangu Mei mwaka 2016.

LFA imekuwa ikipokea kiasi cha kama Pauni milioni 1.16 (sawa na Sh bilioni 3) kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa ajili ya kuendeleza makao makuu yake, ambayo yanakaribia kukamilika, wakati fedha zingine kwa ajili ya kujenga viwanja vinne vidogo katika miji ya Montserrado na Grand Bassa.

Related Articles

Back to top button