Fahyma: “Nilimshonea Wema gauni, nikaishia getini!”

DAR ES SALAAM, Mwanamitindo na mfanyabiashara, Fahyma ‘Fahyvanny’, ambaye pia ni mzazi mwenza wa msanii wa Bongo Fleva Rayvanny, ameweka wazi simulizi ya tukio lililowahi kumkuta alipokusudia kumpatia zawadi staa wa filamu Tanzania, Wema Sepetu.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Fahyma ameeleza kuwa aliwahi kushona gauni maalum kwa ajili ya Wema Sepetu kama ishara ya upendo na heshima.
“Nikawa nimeshona gauni zuri hilo, special kwa ajili ya kwenda kumpa Wema. Nikalishona vizuri kabisa nikamaliza, kisha nikaenda kugonga geti nyumbani kwake,” amesimulia Fahyma.
Hata hivyo, mambo hayakwenda kama alivyotarajia. Alidai alipofika getini na kugonga, alifunguliwa na msichana aliyedhani huenda alikuwa mfanyakazi wa nyumbani.
“Nilivyogonga akafungua msichana, nahisi yule ni beki tatu. Nikamwambia samahani, nina shida na Wema, nina zawadi yake. Akasema amelala, kisha akafunga geti kwa nguvu ‘paaah!’” ameongeza.
Fahyma hakuficha masikitiko yake juu ya tukio hilo, akieleza kuwa dhamira yake ilikuwa njema ya kumkabidhi zawadi hiyo mwenyewe, lakini aliishia kuondoka bila kufanikisha lengo lake.
Simulizi hiyo imeibua mijadala mitandaoni, mashabiki wakitoa maoni yao kuhusu tukio hilo na namna lilivyoshughulikiwa.




