Fadlu ashikilia hatma ya Manula Simba

DAR ES SALAAM: UONGOZI wa klabu ya Simba umesema mapendekezo ya nani anabaki au kuondoka katika eneo la kipa wanategemea na ripoti ya benchi la ufundi linaloongozwa na Fadlu Davids.
Meneja wa idara ya habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema ripoti ya mwalimu ndio yenye mamlaka kwa sababu wao watashauri vipi kuhusu kikosi cha msimu ujao.
Kauli hiyo imekuja baada ya Simba kuwa na makipa watano ambao ni Moussa Camara, Ali Salim, Hussein Abel, Aishi Manula na Ayoub Lakred, jambo linaloonyesha ushindani mkubwa katika nafasi hiyo ya mlinda mlango.
“Manula anamaliza mkataba wake ndani ya Simba na sijajua wakubwa watashauri vipi. Ni kipa mzuri na kutopata nafasi haimuondolei kuwa yeye ni kipa bora,” amesema Ahmed.
Kwa kipindi kirefu, Manula ameihudumia Simba kwa ufanisi mkubwa na kuchangia mafanikio mbalimbali ya klabu hiyo, ikiwemo ubingwa wa ligi kuu na mashindano ya kimataifa. Hata hivyo, msimu huu hakuwa chaguo la kwanza mara kwa mara, hali iliyozua maswali kutoka kwa mashabiki.
Hatma ya Manula sasa iko mikononi mwa benchi la ufundi. Kama ataongezewa mkataba au kuachwa, yote yatategemea tathmini ya kiufundi, hali yake kiafya, kiwango chake cha sasa, pamoja na mipango ya timu kuelekea mashindano ya ndani na kimataifa.