Kwingineko

Enrique amwaga sifa kwa Dembele

EAST RUTHERFORD, Meneja wa Paris St Germain Luis Enrique amesema mshambuliaji wa kikosi hicho Ousmane Dembele ni mtu wa kumtegemea sana hasa wakati huu ambao kikosi chake kinapojiandaa na fainali ya Kombe la Dunia ya Klabu dhidi ya Chelsea, Jumapili baada ya kuichapa Real Madrid 4-0 kwenye nusu fainali jana usiku

Mchezaji huyo anayeongoza mbio za kuwania tuzo Ballon d’Or alikosa michezo ya awali ya hatua nzima ya makundi baada ya kupata jeraha la paja na alilazimika kucheza akitokea benchi katika mechi za 16 bora huku akianza kwa mara ya kwanza katika mchezo huo wa jana usiku.

Dembele aliwaka mapema sana dhidi ya Real akiasisti bao la Fabian Ruiz mnamo dakika ya 6 kabla ya yeye mwenyewe kuingia kambani dakika tatu baadae katika mchezo uliokuwa na hadhi ya fainali uliopigwa Uwanja wa MetLife huko East Rutherford, New Jersey.

Awali Luis Enrique aliwaambia waandishi wa habari kwamba anaamini Dembele anastahili bila shaka tuzo ya Ballon d’Or, na hapo jana akakazia kauli hiyo akisema kwamba hakuna shaka kwamba Mfaransa huyo kwa mara nyingine tena amedhihirisha kuwa anastahili heshima hiyo ya juu ya soka Duniani.

“Ningependa kuwakumbusha kuwa huu ni mchezo wa kwanza kuwa na mchezaji wangu bora Dembele, katika ubora wake. Tumemuona kidogo sana katika michuano hii yote huyu ni mchezaji muhimu, mchezaji wa kipekee, mchezaji ambaye kila shabiki anataka kumuona natumai tunaweza kuwa nae kwa fainali.” Enrique aliwaambia wanahabari.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button