DR Congo yarejea Kombe la Dunia baada ya miaka 52

GUADALAJARA, Mexico: JAMHURI ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) imefuzu kucheza Kombe la Dunia 2026 kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1974, baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Jamaica katika mchezo wa mchujo wa mabara uliochezwa Jumanne usiku.
Bao pekee la ushindi lilifungwa na Axel Tuanzebe katika dakika ya 100 ya muda wa nyongeza, akimalizia mpira wa kona uliosababisha shangwe kubwa kwa mashabiki wa Congo.
Bao hilo lilicheleweshwa kuthibitishwa kwa zaidi ya dakika moja kutokana na ukaguzi wa uwezekano wa kuchezewa kwa mkono, kabla ya mwamuzi kulikubali rasmi.
DR Congo ilionekana kuwa timu bora zaidi katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Estadio Guadalajara nchini Mexico, huku ikitawala sehemu kubwa ya mechi licha ya nafasi chache za wazi za kufunga.
Mshambuliaji wa timu hiyo, Cedric Bakambu, alisema ushindi huo ni wa kihistoria kwa taifa lao.
“Tunafurahi sana, kwa kweli tumefurahi mno. Kwa sasa huenda bado hatujatambua ukubwa wa jambo hili, lakini tutakaporudi Kinshasa kutakuwa na shamrashamra kubwa. Hongera kwa wachezaji wenzangu na kwa Wakongo wote duniani,” amesema Bakambu.
Hii ni mara ya pili kwa DR Congo kufuzu fainali za Kombe la Dunia, baada ya kushiriki kwa mara ya kwanza miaka 52 iliyopita wakati nchi hiyo ilipokuwa ikijulikana kama Zaire.
Kwa ushindi huo, DR Congo imekuwa taifa la 10 kutoka Afrika kufuzu michuano hiyo na sasa itacheza katika Kundi K pamoja na Colombia, Portugal na Uzbekistan.




