Bundesliga

Dortmund yarudi na moto Bundesliga

BERLIN: VIGOGO wa Bundesliga Borussia Dortmund watakuwa wakisaka ushindi wao wa kwanza wa ligi katika michezo mitatu watakapowakaribisha Cologne Jumamosi, wakitumaini mafanikio yao katika Ligi ya Mabingwa Ulaya yatawapa nguvu na kujiamini zaidi.

Klabu hiyo inayotokea eneo la Ruhr jijini Dortmund ilipoteza mechi yao na vinara Bayern Munich katika mchezo wa Der Klassiker wiki iliyopita ikiwa ni kichapo chao cha kwanza msimu huu katika mashindano yote na kushuka hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa Bundesliga, wakiwa pointi saba nyuma ya Bayern.

Hata hivyo, Dortmund walikuwa haraka kujibu mapigo kwenye ushindi wa mabao 4–2 dhidi ya FC Copenhagen katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa usiku wa Jumanne, ushindi uliorejesha morali ndani ya kikosi hicho.

Ilikuwa ni mechi yao ya tatu mfululizo kwenye Ligi ya Mabingwa ambayo walifunga mabao manne, huku wakionesha soka la kasi na mashambulizi ya kuvutia. Hadi sasa, wana safu ya pili bora ya mashambulizi katika michuano hiyo, wakiwa na pointi saba ambazo zimewaweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya16 bora.

Lakini kwenye Bundesliga, safari yao imekuwa na misukosuko baada ya kutoka sare na RB Leipzig walioko nafasi ya pili kabla ya kupoteza dhidi ya Bayern. Baada ya mchezo wa nyumbani dhidi ya Cologne, Dortmund wanakabiliwa na michezo minne mfululizo ya ugenini katika Kombe la Ujerumani, Ligi ya Mabingwa, na Bundesliga hali inayohitaji umakini mkubwa.

“Kwa ujumla, tunahisi timu ipo imara, Lakini ili kuthibitisha hilo, tunahitaji matokeo. Tuliyapata tena kule Copenhagen, jambo linalotupa kujiamini na kuonesha kuwa hata wachezaji wapya au wa akiba wana ubora mkubwa utakaotusaidia katika wiki zijazo.” alisema Mkurugenzi wa Michezo wa Dortmund, Sebastian Kehl.

Katika hatua nyingine mwingine, kocha wa kikosi hicho Niko Kovac amesifiwa kwa kuimarisha uimara wa safu ya ulinzi ya timu hiyo pamoja na kuboresha uthabiti wa mashambulizi tangu alipoanza kuinoa katikati ya msimu uliopita.

“Tunataka kucheza soka la kushambulia na kuwabana wapinzani, tukiwalazimisha kufanya makosa. Inafanya kazi vizuri katika Ligi ya Mabingwa. Kwenye Bundesliga hatujaridhika kabisa, lakini bado mambo yanaweza kuwa bora zaidi. Bila shaka ningependa kuona nafasi zaidi za wazi na mabao mengi zaidi. Lazima uwe na uimara nyuma ili kupata ubora mbele ya lango.” – amesema Kovac.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button