Donnum achunguzwa kwa ubaguzi

PARIS: WINGA wa Toulouse, Aron Donnum, yuko chini ya uchunguzi wa awali kufuatia tuhuma za kuonesha ishara ya kibaguzi, kwa mujibu wa ofisi ya mwendesha mashtaka wa Toulouse, kama alivyoliambia shirika la Reuters Alhamisi, baada ya taarifa za awali kutoka kwenye gazeti la L’Equipe la Ufaransa.
Uchunguzi huo unatokana na tukio lililotokea katika mechi ya Ligue 1 kati ya Toulouse na Le Havre tarehe 2 Novemba, ambapo Donnum ambaye amekanusha vikali tuhuma hizo alipunga mkono mbele ya pua yake akiwa anamuelekea kiungo wa Le Havre, Simon Ebonog, raia wa Cameroon.
“Itakuwa vizuri kuweka wazi kwamba mfumo wa sheria utafuatilia kikamilifu vitendo vyote vya ubaguzi wa rangi. Waziri wa Sheria ametoa mwongozo mpya unaosisitiza umuhimu wa kupambana na makosa kama haya, ambayo yanadhoofisha misingi ya maadili ya Jamhuri yetu,” – mwendesha mashtaka David Charmatz ameiambia Reuters.

Kocha wa Le Havre, Didier Digard, alikosoa vikali kitendo hicho mara baada ya mechi hiyo kumalizika. “Kuna tafsiri gani nyingine? Kama mtu ananiambia siyo ubaguzi, basi ni nini?” alihoji.
Donnum, kwa upande wake, alisema baada ya mchezo huo kuwa hatua yake haikuwa na uhusiano wowote na ubaguzi wa rangi, huku klabu ya Toulouse ikitoa taarifa ya kulaani kwa nguvu zote tuhuma zisizo na msingi.
Tume ya nidhamu ya LFP inatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu sakata hilo Jumatano ijayo.




