
AGOSTI 22, 1972, Sonny Wortzik, rafi ki yake Sal Naturale na Stevie wanaingia katika Benki ya Akiba ya Brooklyn ili kuiba.
Wakiwa humo benki mpango wao unaenda mrama baada ya mwenzao Stevie kupoteza ujasiri na kutoka nduki, na muda huo huo Sonny anagundua kuwa wamechelewa kwani fedha walizozihitaji zimekwisha chukuliwa, na hivyo wanaambulia dola 1,100 tu.
Sonny anabeba hundi za wasafiri za benki na kisha anachoma moto rejesta, lakini moshi unaofuka unawafanya watu walio nje ya jengo la benki kushtuka, na mara jengo linazingirwa na polisi.
Sonny na Sal wanaogopa na kuwateka wafanyakazi wa benki. Mpelelezi wa Polisi, Sajenti Eugene Moretti anawataka wajisalimishe, Sonny anadai kuwa yupo tayari kuwa mateka lakini si kujisalimisha.
Sal anamhakikishia Sonny kwamba hata yeye yupo tayari kwa lolote. Kwa hofu mlinzi wa benki hiyo anabanwa na pumu, Sonny anamwachia kama ishara ya upendo. Wakati huo Sajenti Moretti anajaribu kumshawishi Sonny kujisalimisha.
Akimtumia mtoa fedha mkuu kama ngao, Sonny anaanzisha majadiliano na Sajenti Moretti ambayo yanaishia katika kelele za “Attica! Attica!” kuomba uchunguzi wa vurugu katika jela ya Attica, na umati unamshangilia Sonny.
Sonny anatoa masharti kuwa aletewe gari litakalowapeleka kiwanja cha ndege. Pia anadai ziletwe pizza kwa ajili ya mateka, na kwamba mkewe aletwe hapo benki.
Mke wa Sonny, bibie Elizabeth Shermer anafika na kueleza kwamba wizi huo ulikuwa na nia ya kutafuta fedha za kulipia matibabu yake ya upasuaji wa maumbile yake ya kike. Anafafanua kuwa mumewe Sonny ana watoto kwa mke waliyetengana, Angie.
Hatimaye usiku unaingia, taa za benki zinazimwa na mpelelezi wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), Sheldon anaweka ulinzi mkali katika eneo hilo.
Sheldon anayakataa masharti ya Sonny lakini meneja wa benki hiyo, Mulvaney anapoingia ndani ya jengo anapatwa na mshtuko, na hivyo Sheldon anamruhusu daktari aingie.
Baada ya matibabu Sonny anamruhusu meneja aondoke lakini anakataa kuwaachia wafanyakazi wengine wa benki. FBI wanamtaka Sonny atoke ili kuzungumza na mama yake ambaye bila mafanikio anajaribu kumshawishi ajisalimishe.
Ndani, Sonny anaandika wosia kwamba, fedha kutoka kwenye bima yake ya maisha
zisaidie upasuaji wa mkewe Elizabeth na zingine apewe mtalaka wake, Angie.
Baadaye gari aina ya Limousine linafika ili kuwachukua Sonny na Sal, Sonny anachunguza kila upande kuona kama kuna bunduki au mitego iliyofichwa ili kuwamaliza, na kumtaka mpelelezi Murphy awaendeshe.
Kisha anaingia yeye, Sal na mateka hadi kiwanja cha ndege cha John F. Kennedy. Sonny akiwa ameketi mbele kabisa kando ya mpelelezi Murphy na Sal ameketi nyuma akiwa amemwelekezea Murphy mtutu.
Mpelelezi Murphy anamtaka Sal mara kwa mara kuelekeza bastola yake kwenye paa ili asije kumpiga risasi kwa bahati mbaya. Wakati wanasubiri kwenye lami ya kiwanja cha ndege, Sal anamwachia mateka mwingine wa kike, ambaye anamzawadia rozari yake.
Mpelelezi Murphy anamwomba tena Sal kuelekeza bastola yake kando. Sal anafanya kosa kubwa kukubali, na nafasi hiyo inatumiwa vyema na wapelelezi Sheldon na Murphy. Katika purukshani hiyo Sal anapigwa risasi ya kichwa na Sonny anawekwa chini ya ulinzi, huku mateka wote wakiachiwa huru.
Filamu inaisha wakati Sonny anauangalia mwili wa Sal ukichukuliwa kutoka kwenye gari kwa machela. Maandishi yanaonesha kwamba Sonny alihukumiwa kifungo cha miaka 20 gerezani, mwanamama Angie na watoto wake walisaidiwa na ustawi wa jamii, na bibie Elizabeth alifanyiwa upasuaji.
Filamu hii inasimulia kisa cha ukweli kinachomhusu John Wojtowicz, kwa mujibu wa makala iliyowahi kuchapishwa katika jarida la LIFE mnamo Septemba 22, 1972 yenye kichwa “The Boys in the Bank”.
Wojtowicz, akiwa na Sal Naturale, walivamia tawi la benki la Chase Manhattan huko Gravesend, Brooklyn, Agosti 22, 1972. Walipokamatwa, Wojtowicz alihukumiwa miaka 20 jela, na alitumikia kifungo cha miaka sita akaachiwa.
Baada ya filamu hii kutoka mwaka 1975, Wojtowicz aliandika barua The New York Times akidai kuwa matukio ndani ya filamu hii yalikuwa na “ukweli wa asilimia 30 tu”.
Hoja yake ilikuwa kukosekana kwa usahihi wa mambo kama suala la mtalaka wake, ambaye jina lake halisi aliitwa Carmen Bifulco, mazungumzo kati yake na mama yake na polisi kukataa kumruhusu kuongea na Carmen (Angie).
Hata hivyo, aliwamwagia sifa waigizaji Al Pacino na Chris Sarandon kwa kuwaigiza vyema yeye na Elizabeth Eden. Pia, ingawa Sal alikuwa na umri wa miaka 18 wakati wa jaribio la wizi huo, kwenye filamu hii nafasi yake imechezwa na John Cazale mwenye umri wa miaka 39.
0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com