Dk Biteko atoa maagizo makali kusuasua SHIMMUTA

DODOMA: Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko amemuagiza Msajili wa Hazina kufikia Jumanne Novemba 21, 2023 awasilishe taarifa kwa nini mashirika mengi ya Serikali hayajatoa kibali kwa watumishi wao kushiriki Mashindano ya Taasisi, Mashirika ya Umma na Binafsi (SHIMMUTA) mwaka 2023 jijini Dodoma.
Biteko ametoa maagizo hayo wakati akifungua mashindano hayo Novemba 17, 2023 Uwanja wa Jamhuri Dodoma ambapo amebaini mashirika ya umma yapatayo 248 nchini hayakushiriki mashindano hayo huku mashirika 54 pekee ndio yametoa kibali kwa watumishi wao kushiriki mashindano hayo.
“Naipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuendelea kusimamia vyema michezo, kwa sasa tunashuhudia nchi yetu ikitangazwa vyema na hivi karibuni tumepata uwenyeji wa Mashindano ya AFCON mwaka 2027 kwa kushirikiana na wenzetu wa Kenya na Uganda”Dk Doto Biteko.
Dk Biteko amewaasa wanamichezo hao kutumia michezo hiyo kubadilishana uzoefu, kupeana mbinu za mafanikio lakini pia kujifunza kuweka alama mahali wanapofanyia kazi pamoja na kutimiza wajibu wa kuhakikisha wanatatua matatizo ya wananchi kupitia sehemu za kazi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma amezipongeza Taasisi za Serikali, Mashirika ya Umma na Binafsi yaliyotoa ruhusa kwa Watumishi kushiriki mashindano hayo, akisema ni hatua nzuri ya kuunga mkono serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuendeleza michezo nchini.
“Katika kipindi hiki cha serikali ya awamu ya sita, tumeshuhusia maendeleo makubwa katika sekta ya michezo ikiwemo kupata uwenyeji wa Mashindano ya AFCON mwaka 2027, Klabu ya Simba kucheza hadi robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2022/ 23 na Klabu ya Yanga kucheza hadi fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2022/23” amesema Mwinjuma.
Aidha, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Gerson Msigwa amesema lengo la mashindano hayo ni kuimarisha afya za watumishi na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, huku akitoa rai kwa makampuni, taasisi za serikali na binafsi kutekeleza maelekezo hayo.