Aussems kuisuka Singida Black Stars ya moto
DAR ES SALAAM: KOCHA mkuu mpya wa Singida Black Stars, Patrick Aussems maarufu Uchebe amesema malengo makubwa ni kuona timu hiyo inakuwa katika tatu au nne bora katika Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024/25.
Amesema kama anahitaji kufanya vizuri ni lazima kuwepo kwenye nafasi hizo ili baadae kuja kuleta ushindani kwa klabu kongwe hapa nchini za Simba na Yanga.
Ameyasema hayo jijini Dar Es Salaam, katika mkutano maalum na waandishi wakati akitambulishwa kama kocha mkuu wa timu hiyo yenye maskani yake mkoani Singida, amesema anaifahamu ligi ya Tanzania na kikubwa kushinda mechi zao.
Aidha amesema hafikirii kushindana na klabu kongwe za hapa nchini, zaidi anatamani kuona timu yake ifanye vizuri na kufika katika nafasi tatu za juu na kutafauta matokeo kwa timu hizo mbili.
“Nafurahia kuwepo Tanzania, baada ya kuondoka nilikuwa Afrika kusini na msimu uliopita nilikuwa Kenya, nilikuwa na ofa nyingi lakini nimeridhishwa na mipango ya Singida Black Stars na kusaini mkataba wa kuinoa timu hiyo”.
“Ninaimani kubwa ya kufanya vizuri ndani ya Singinda Black Stars, Ulaya ukaitaja Tanzania kila mtu anawaza kuhusu Simba, najua wengi mtasema vipi kuhusu yanga ila ukweli ni huo kwa sasa nataka timu hiyo nayo kufahamika Ulaya kama ilivyo kwa klabu hiyo kongwe,” amesema Kocha huyo.
Nae Mtendaji Mkuu wa Singida Black Stras, Jonathan Kasano amesema kocha amewasili nchini kuanza kazi rasmi ya kukinoa kikosi cha Singida BS kwa msimu ujao wa Mashindano.
“Tumebadili ratiba yetu ambayo kambi tulipanga kuweka Arusha lakini kwa michuano ya Kagame tunalazimika kubaki Dar es Salaam kufanya maandalizi ya msimu ujao,” amesema Kasano.
Amesema wamemtambulisha rasmi Aussems na kumkabidhi mipango yao ya miaka mitatu ijayo ikiwemo kuleta ushindani mkubwa ndani ya ligi ya Tanzania.