Muziki

DJ Khaled: Nisaidieni kumsihi Rihanna ashiriki katika albamu yangu

MCHEZA diski maarufu nchini Marekani DJ Khaled amewataka mashabiki kumfikishia ujumbe wake mwanamuziki Rihanna ili aweze kushiriki katika albamu yake ijayo.

Mkali huyo wa ‘Another One’ alitoa ombi hilo wakati akitokea kwenye kipindi cha ‘Tonight Show’ kilichoandaliwa na Jimmy Fallon hivi karibuni.

Khaled alifichua kuwa alituma rekodi ambayo alitaka Rihanna amshirikishe lakini hakukuwa na jibu hivyo amewaomba mashabiki wake wamsaidie kumbembeleza na kumshawishi mwanadada huyo akubali kushiriki katika wimbo huo.

“Nimemtumia tu Rihanna rekodi ambayo nataka ashiriki. Nahitaji ninyi nyote mnisaidie kufikisha ujumbe huu kwake,” aliomba Dj Khaled hadhira.

Albamu ijayo ya 14 ya DJ Khaled, ‘Til Next Time,’ inatarajiwa kuachiwa ndani ya mwaka huu.

Nyota huyo wa muziki alifichua katika mahojiano na Rolling Stone mwaka jana kwamba mwimbaji wa Nigeria aliyeshinda Grammy, Burna Boy atakuwa kwenye albamu hiyo.

Rihanna, kwa upande wake alikuwa amepumzika kimuziki na katika miaka ya hivi karibuni alitoa wimbo uliotumika katika filamu wa Black Panther 2, ‘Lift Me Up,’ ambao uliandikwa na mwimbaji wa Nigeria aliyeteuliwa na Oscar, Temilade Openiyi, anayejulikana zaidi kama Tems.

Related Articles

Back to top button