Dalali: Wahujumu Simba wasithubutu kukanyanga New Amaan Complex

ZANZIBAR: KATIKA kilele cha maandalizi ya mechi ya marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC) kati ya Simba SC na RS Berkane, aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali, ametuma ujumbe mzito kwa wale wanaodaiwa kupanga hujuma dhidi ya timu hiyo.
Simba, ambayo itakuwa mwenyeji katika mechi hiyo itakayopigwa kwenye dimba la New Amaan Complex visiwani Zanzibar, ina matumaini makubwa ya kutwaa ubingwa huo wa kihistoria.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa hamasa kuelekea mechi hiyo uliofanyika leo Zanzibar, Dalali alisema: “Tuna taarifa kamili kuhusu wale wanaopanga kuihujumu Simba, iwe wako Bara au Visiwani. Nawatahadharisha wasithubutu hata kufika uwanjani. Kama Simba hawatashinda kutokana na hujuma, hatutamwacha mtu salama, awe ndani au nje ya Simba. Tutamshughulikia.”
Dalali alikumbusha tukio la kihistoria mwaka 1993 ambapo Simba walidaiwa kuhujumiwa wakati wa fainali, mbele ya aliyekuwa Rais wa awamu ya pili, Hayati Ali Hassan Mwinyi, hali iliyosababisha kikombe kuchukuliwa na wageni.
“Mwaka huo tulihujumiwa. Sasa mnakuja tena, wakati mgeni rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi? Mtu na baba yake wanahujumiwa? Hamchoki? Safari hii hatukubali. Kombe lazima libaki nyumbani,” amesema .
Dalali amesisitiza kuwa wale wanaoiombea mabaya Simba hawana nafasi kwenye uwanja huo, kwani Simba hawawakilishi klabu pekee bali taifa zima.
“Anayehujumu Simba ni msaliti wa taifa. Rais Samia Suluhu Hassan anatoa fedha nyingi kupitia ‘Goli la Mama’ kusaidia michezo. Tunawamudu RS Berkane hapa nyumbani,” ameongeza.
Kwa mujibu wa Dalali, tayari ameongea na wachezaji na wote wamemhakikishia kuwa wanatamani kulibakiza kombe hilo nyumbani. Mashabiki wa Simba wawaunge mkono vijana. Wanahitaji sapoti, wapo tayari kupambana kwa ajili ya Simba na kwa heshima ya taifa.