Nyumbani

Saido ala talaka tatu Simba

DAR AS SAALAM: UONGOZI wa Simba umetangaza rasmi kuachana na aliyekuwa kiungo wao, Saidi Ntibanonkiza, baada ya nyota huyo kutoongezewa mkataba mwingine baada ya awali kufikia tamati.

Kwa misimu miwili Saido amekuwa kinara wa kufumania nyavu ndani ya kikosi cha Simba, kwa msimu huu alimaliza akiwa na mabao 11 sawa na Max Zengeli na msimu wa 2022\23 waligongana katika ufungaji na aliyekuwa staa wa Yanga Fiston Mayele wakiwa na mabao 17.

Saido ni mchezaji wa pili kupewa ‘Thank You’ ndani ya kikosi cha timu hiyo baada ya jana kutangaza John Bocco kutokuwa sehemu ya kikosi cha wekundu wa msimbazi kwa msimu 2024\25.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Meneja wa Idara ya habari na Mawasiliano, Ahmed Ally imesema Saido hatokuwa sehemu ya kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao baada ya kumaliza mkataba wake.

Amesema kipindi cha mwaka mmoja na nusu alichodumu na Simba akitokea Geita Gold FC, kiungo huyo amekuwa mchezaji muhimu wa kikosi cha kwanza akiwa mfungaji bora katika misimu yote miwili.

“Tunathamini mchango wake, tukumbuke msimu 2022\23 alikuwa mfungaji bora baada ya kufunga mabao 17 pia aliibuka kiungo bora wa msimu, licha ya kucheza kwa muda mfupi, Saido ameacha alama ndani ya kikosi hicho kutokana na utumishi uliotukuka ndani na nje ya uwanja,” imesema taarifa iliyotolewa na simba.

Imesema uongozi wa klabu unamtakia kheri kiungo huyo katika Maisha yake mapya ya soka nje ya kikosi cha wekundu wa msimbazi. kuachana na nyota huyo ni hatua za klabu hiyo kuendelea kufanya maboresho makubwa ya kikosi kwa ajili ya msimu ujao.

Related Articles

Back to top button