Conte ajaa ‘minoti’ Napoli

NAPLES:MABINGWA wa Serie A SSC Napoli wametoa ofa ya nyongeza ya mshahara kwa Antonio Conte ili aendelee kusalia katika klabu hiyo wakikwepa uwezekano wa raia huyo wa Italia kurubuniwa na klabu nyingine hasa baada ya kuiwezesha Napoli kuwa Mabingwa msimu uliomalizika.
Taarifa kutoka katika viunga vya jiji la Napoli zinaeleza kuwa mpango huo kabambe uliwasilishwa na mmiliki wa klabu hiyo Aurelio De Laurentiis kwani Napoli wanataka kumbakisha Conte kwa gharama yoyote ile kwa msimu ujao labda na misimu mingine zaidi.
Uwekezaji mkubwa sokoni huku majina makubwa kama Kevin De Bruyne yakitajwa pamoja na ongezeko la mshahara huo kwa Conte ni wazi Napoli hawataki mchezo kabisa msimu ujao. Klabu inaamini kuendelea na Conte, mpango kabambe unaoeleweka huku Napoli ikisubiri uamuzi rasmi wa Antonio Conte
Conte alichukua mikoba ya kuinoa timu hiyo majira yaliopita aa joto na kuiongoza kutoka nafasi ya 10 waliomaliza msimu wa 2023/24 hadi kuwa mabingwa wa taji la Serie A msimu uliomalizika.
Mtaalamu huyo wa Kiitaliano, ambaye pia amebeba taji la ‘Scudetto’ mara tano kama kocha, bado ana mkataba na Napoli hadi 2027. Conte na De Laurentiis walikutana Jumanne jijini Rome, na kocha huyo anatumia siku kadhaa kufikiria mustakabali wake baada ya mkutano huo.