Ligi Ya Wanawake

Clara Luvanga hashikiki Saudi Arabia

RIYADH: NYOTA wa Twiga Stars, Clara Luvanga, anaendelea kuonesha kiwango cha juu katika Ligi Kuu ya Wanawake Saudi Arabia baada ya kuongoza orodha ya wafungaji bora hadi kufikia raundi ya 10 ya michuano hiyo.

Mshambuliaji huyo hatari tayari ameshafunga mabao 18, akimuacha mbali mpinzani wake wa karibu Adriana Silva mwenye mabao 12, huku Leale Garrec wa Al Qadsiah akifunga 11.

Wengine wanaomfuatia ni Ibtissam Jraidi mwenye mabao 10 na Naomie Kabakaba wa Al Ahli aliyefunga mabao nane.

Luvanga pia ana mchango mkubwa kwa timu yake ambayo inaendelea kufanya vizuri kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 30 baada ya kushinda michezo yote 10.

Mbali na kuongoza ligi, timu hiyo pia ina rekodi bora ya ushambuliaji kwa kufunga mabao 43 huku ikiruhusu mabao nane pekee, jambo linaloonesha ubora wao katika mashambulizi na ulinzi.

Kwa kiwango hiki, Luvanga anaendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa na kuthibitisha kuwa ni miongoni mwa washambuliaji hatari zaidi kwa sasa.

Related Articles

Back to top button