Chelsea yazomewa ikitinga nusu fainali ya UEFA ECL

LONDON, Wenyeji wa Stamford Bridge Chelsea FC walijipata katika wakati mgumu wakati kikosi hicho kilipoambulia kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa klabu ya Legia Warsaw ya nchini Poland katika mchezo wa pili wa Robo Fainali ya UEFA Europa Conference League nyumbani jana usiku.
Mashabiki wa klabu hiyo walikuwa wakiwazomea wachezaji wao katika kile kinachoonekana kama mwenendo usioridhisha wa klabu hiyo katika michezo yake ya hivi karibuni na jinsi walivyopoteza mchezo huo ambao walikuwa wameukamata kwa kipindi chote madai ambayo yaliungwa mkono na nahodha wa kikosi hicho Reece James.
James alisema walizembea baada ya kuona wana uongozi wa jumla wa mabao 3-0 uzembe ambao ungeweza kuwagharimu kuondolewa kwenye michuano hiyo kama matokeo ya mchezo wa kwanza yangekuwa tofauti.
“Tulikuwa na Uongozi wa jumla wa 3-0 labda hiyo ilitufanya tuzembee kidogo, tunapiga hatua lakini sidhani kama uzembe ule ni miongoni mwa hatua hizo. Labda hatuuheshimu mchezo na michuano ambayo usipojiandaa vyema itatugharimu”
“Itaharibu ‘mindset’ yetu hili litabaki vichwani kwa muda mrefu. Naelewa hasira yao, mahabiki wamekuja uwanjani kupata furaha badala yake tumewakera” alisema Reece James.
Wachambuzi wa soka nchini England wanaamini Chelsea inapaswa kubadilika kuelekea mchezo muhimu wa Dabi ya London magharibi dhidi ya Fulham Jumapili ikiwa kikosi hicho kinataka kuwania nafasi katika nafasi 5 za kufuzu moja kwa moja kwa Ligi Ya Mabingwa msimu ujao.
Chelsea watakutana na klabu ya Djurgarden kutoka nchini Sweden kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo baada ya klabu hiyo kuiondoa Rapid Wien ya Austria kwa jumla ya mabao 4-2.