
LONDON:KLABU ya Chelsea imemtangaza rasmi Liam Rosenior kama kocha mkuu mpya wa timu hiyo, akitia saini mkataba wa miaka sita utakaomweka Stamford Bridge hadi mwaka 2032.
Rosenior mwenye umri wa miaka 41 anachukua nafasi ya Enzo Maresca aliyeondoka Chelsea siku ya Mwaka Mpya. Kupitia taarifa yao, Chelsea wamesema msisitizo utaendelea kuwa kwenye kukuza na kuendeleza wachezaji, huku wakisisitiza kuwa matarajio na malengo ya klabu bado yako juu.

Akizungumza baada ya kutangazwa, Rosenior amesema kuaminiwa kupewa nafasi hiyo ni heshima kubwa kwake na ameahidi kutoa kila kitu kwa ajili ya mafanikio ya klabu. “Hii ina maana kubwa sana kwangu. Nitatoa kila nilichonacho kuiletea Chelsea mafanikio,” amesema. Ameongeza pia, “Nitapenda klabu yangu ya zamani maisha yangu yote, lakini nisingeweza kuikataa Chelsea,naamini hata wao watajivunia hilo.”
Mchezo wake wa kwanza rasmi utakuwa dhidi ya Charlton kwenye FA Cup, Jumamosi hii. Rosenior ataambatana na benchi lake la ufundi lililojumuisha Khalifa Cisse, Ben Warner na Justin Walker, akianza safari mpya yenye presha na matarajio makubwa kutoka kwa mashabiki wa Blues.




