Chelsea yakubali ombi la Arsenal kumsajili Jorginho

KLABU ya Arsenal ‘The Gunners’ imekubali dili na Chelsea kumsajili kiungo wa Italia, Jorge Luiz Frello Filho Cavaliere OMRI maarufu Jorginho kwa ada ya pauni milioni 12 sawa na shilingi bilioni 34.5.
Jorginho mwenye umri wa miaka 31 aliyejiunga na Chelsea mwaka 2014 akitokea Napoli yupo katika miezi sita ya mwisho ya mkataba wake Stamford Bridge.
Atafanyiwa vipimo kabla ya kusaini mkataba wa miezi 18 wenye chaguo la nyongeza ya mwaka mmoja.
The Gunners imegeukia kwa Jorginho baada ya maombi mawili ya kumsajili Moises Caicedo wa Brighton & Hove Albion kukataliwa.
Jorginho anakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa katika dirisha la Januari baada ya beki wa Poland Jakub Kiwior kwa pauni milioni 17.6 sawa na shilingi bilioni 50.6 na mshambuliaji wa Ubelgiji Leandro Trossard aliyehama kutoka Brighton kwa pauni milioni 21 sawa na shilingi bilioni 60.3.
Jorginho amefunga mabao 29 katika michezo 213 aliyecheza Chelsea akishinda Ligi ya Mabingwa, Ligi ya Europa, Uefa Super Cup na Kombe la Dunia la Klabu kipindi akiwa klabu hiyo.
Kiungo huyo alizaliwa Brazil lakini alihamia Italia akiwa na umri wa miaka 15 na kuchagua kucheza timu ya Taifa ya Italia ‘Azzurri michezo ya kimataifa.