CHAN

CHAN 2025, Ufunguzi kwa Mkapa, fainali Kenya

DAR ES SALAAM: MASHINDANO ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2025 yanazidi kunukia baada ya Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kutangaza viwanja vitakavyotumika kwa mechi muhimu, ikiwemo ya ufunguzi, mechi ya mshindi wa tatu, na fainali.

Kwa mujibu wa CAF, mechi ya ufunguzi ya michuano hiyo itapigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, Tanzania, Jumamosi ya Agosti 2, 2025. Huu ni uamuzi unaoonyesha kuipa heshima Tanzania kama mmoja wa wenyeji wa mashindano haya kwa mara ya kwanza.

Aidha, mechi ya kutafuta mshindi wa tatu itafanyika katika Uwanja wa Mandela uliopo Kampala, Uganda, huku fainali ya michuano hiyo ikipangwa kuchezwa katika Uwanja wa Kasarani, Nairobi, Kenya, tarehe 30 Agosti 2025.

Katika kuhakikisha mashindano haya yanashirikisha maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki, Zanzibar nayo imepewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa baadhi ya mechi, hatua ambayo imepongezwa kwa kuonyesha dhamira ya CAF kupanua ushirikishwaji wa soka barani Afrika.

Uwanja wa Amaan, Zanzibar, ambao hivi karibuni uliandaa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Simba na RS Berkane, umepewa jukumu la kuwa sehemu ya mashindano haya makubwa ya bara.

CAF pia imetangaza miji itakayopokea mechi za hatua ya makundi ambapo kundi A litachezwa Nairobi, Kenya na linajumuisha timu za Kenya, Morocco, Angola, DR Congo na Zambia.

Kundi B litapigwa Dar es Salaam, Tanzania na litawakutanisha wenyeji Tanzania pamoja na Madagascar, Mauritania, Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).

Kwa upande wa Kampala, Uganda, mji huo utakuwa mwenyeji wa kundi C ambalo lina timu za Uganda, Niger, Guinea, Afrika Kusini na Algeria.

Zanzibar imepangwa kuchezwa kwa mechi za kundi D ambalo linajumuisha mataifa makubwa kama Senegal, Congo, Sudan na Nigeria, jambo linaloashiria mechi kali na ushindani mkali visiwani humo.

Katika mabadiliko ya hivi karibuni, Kamati ya Rufaa ya CAF imetangaza kuiondoa Equatorial Guinea kwenye mashindano na nafasi hiyo kuchukuliwa na timu ya Congo, ambayo sasa imeingizwa rasmi kwenye kundi D.

Hatua hii ya CAF ni ushahidi wa maandalizi madhubuti na dhamira ya kuhakikisha CHAN 2025 inakuwa ya kipekee kwa kushirikisha mataifa mbalimbali na kutumia miundombinu bora iliyopo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button