‘C’est Jésus’ ya Nana Miriam yatua Novemba 16

DAR ES SALAAM: MWANAMUZIKI chipukizi wa Injili kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Nana Miriam, anaendelea kuthibitisha ubora wake katika muziki wa kuabudu baada ya kutambulisha rasmi kionjo cha wimbo wake mpya, C’est Jésus, aliouimba kwa kushirikiana na mwimbaji maarufu Sylvain Kashila.
Akizungumza na Spoti Leo Nana amesema kupitia kolabo hiyo, wawili hao wamezua msisimko mkubwa miongoni mwa mashabiki wa muziki wa Injili nchini Kongo, huku wengi wakisubiri kwa hamu kuisikia toleo kamili la wimbo huo linalotarajiwa kutoka rasmi Novemba 16, mwaka huu.
C’est Jésus ni wimbo unaoelezea upendo wa Mungu na nguvu ya jina la Yesu katika maisha ya mwanadamu ujumbe ambao kwa mujibu wa Nana Miriam, unalenga kuwapa watu tumaini na imani katika nyakati ngumu.
“Wimbo unatoka wiki ijayo, Novemba 16. Naomba mashabiki wetu wa hapa Kongo, Tanzania na sehemu nyingine duniani wakae karibu na mitandao yetu ya kijamii. Video itakapotoka, tupe sapoti ili kolabo yetu C’est Jésus ifike mbali,” amesema kwa furaha Nana Miriam.
Kwa sasa, kipande kifupi cha wimbo huo kimeanza kusambaa kwenye majukwaa ya kidijitali, kikionyesha ubunifu, sauti tamu na uimbaji wenye nguvu unaoashiria kuwa C’est Jésus huenda ikawa moja ya nyimbo zitakazotikisa muziki wa Injili mwaka huu.




