BSS kuja kivingine,mshindi kuondoka na milioni 50 na gari

DAR ES SALAAM:MSIMU wa 16 wa tamasha la kusaka vipaji la Bongo Star Search (BSS) Next Level Revolution mwaka huu umebeba sura mpya, likitarajiwa kuanza rasmi Novemba 22, 2025 mkoani Mwanza katika ukumbi wa La Kailo Hotel. Mshindi wa kwanza wa msimu huu ataondoka na zawadi ya Shilingi milioni 50 pamoja na gari jipya.
Akizungumza na SpotiLeo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa shindano hilo, Madam Rita Paulsen, amesema kuwa msimu huu utakuwa wa kipekee kwa kuwa utaangazia vipaji vyote ikiwemo uimbaji, uchoraji, sarakasi, uchekeshaji, upigaji vyombo na uchezaji.

“Nimesimama kwa heshima kubwa na furaha isiyoelezeka kutambulisha rasmi msimu wa 16 wa Bongo Star Search msimu mpya wenye sura mpya, nguvu mpya na dira mpya,” amesema Madam Rita.
“Pia ninayo furaha kutangaza rasmi ushirikiano wetu wa kimkakati kati ya Benchmark 360 na Azam Media, ambao tunauita ‘ndoa ya maono’ maono ya kukuza, kuinua na kuangaza vipaji vya Afrika Mashariki na Kati kupitia jukwaa la BSS,” ameongeza.
Madam Rita alisema kuwa mwaka huu washiriki watatoka ndani na nje ya Tanzania, ikiwemo nchi za Kenya, Uganda, Congo, Malawi, Rwanda na Burundi.
Kwa upande wa Tanzania, mchujo wa awali utafanyika katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Mbeya na Dar es Salaam, kuanzia Novemba 22 hadi 23 mkoani Mwanza, na Novemba 29 hadi 30 mkoani Arusha.
Naye Afisa Mwendeshaji wa Mahudhui na Utangazaji wa Azam Media, Yahya Mohamed, amesema shindano hilo ni sehemu ya dhamira ya Azam Media kuendelea kutoa burudani bora kwa jamii.
“Bongo Star Search Next Level Revolution ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kuhakikisha burudani inawafikia Watanzania popote walipo,” amesema Yahya.
Shindano hilo litarushwa mubashara kupitia chaneli ya Sinema Zetu kwenye ving’amuzi vya Azam, kila Jumapili saa 3 usiku.




