Mastaa

Bob Junior ataka maua yake akiwa hai

DAR ES SALAAM: MSANII wa Bongo Fleva, Raheem Rummy maarufu kama Bob Junior, amefunguka kuhusu changamoto anazopitia katika tasnia ya muziki na kukosa kutambuliwa ipasavyo licha ya mchango wake mkubwa.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Bob Junior ameeleza kuwa amekuwa sehemu muhimu ya historia ya muziki wa Bongo Fleva, si tu kama msanii bali pia kama producer aliyeibua vipaji vingi vikubwa nchini.

“Nimepitia kwenye muziki nikiwa na historia kubwa kuwa kama msanii kisha kuwa kama producer, nakutoa vipaji vingi vikubwa. Ila heshima yangu napewa, lakini nastahili heshima kubwa zaidi. Makubwa niliyofanya na niliowafanyia hawataki kusema moja kwa moja,” ameandika Bob Junior.

Msanii huyo ameongeza kuwa ni tabia ya binadamu wengi kusubiri mtu afe ndipo waanze kumpa sifa, jambo alilolieleza kuwa ni unafiki.

“Huwa binadamu wanasubiri mpaka mtu afe ndo apewe sifa zake. Nachosema tuwe wanadamu wakweli — kama mtu ana stahili makubwa aliyofanya, tusisubiri mpaka afe ndio tuseme mazuri yake. Ni unafiki, ni hayo tu,” ameongeza.

Ikumbukwe kuwa kwa sasa Bob Junior anasumbuliwa na matatizo ya afya, ikiwemo changamoto ya moyo na tatizo la jicho linalohitaji upasuaji nchini India.

Related Articles

Back to top button