BMT, Twalipo kuendeleza ushirikiano

DAR ES SALAAM, Katibu Mtendaji wa baraza la michezo nchini BMT Neema Msitha ameiomba Shule ya mafunzo ya michezo na utimamu wa mwili kupitia kwa Mkuu wake Kanali John Thomas Nyanchoha pamoja na wakufunzi wa Michezo kutoka kambi ya Twalipo Mgulani kuendelea na ushirikiano na Baraza pamoja na vyama vya michezo nchini.
Msitha amesema hayo, leo Machi 19, 2025 wakati Kanali Nyanchoha na wenzake walipomtembelea Ofisini kwake jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumuaga kama mdau wao Mkuu wa Michezo nchini wanayeshirikiana naye, wakieleza kuhamisha shule hiyo kuelekea ‘Sokoine Barracks’ Wilaya ya Monduli mkoani Arusha.
Akizungumza ofisini hapo Msitha amesema BMT na serikali kwa ujumla inalitegemea sana jeshi hilo katika kuzalisha vipaji vya wanamichezo nchini ambao kwa kiwango kikubwa wameiletea nchi heshima kubwa.
“Sisi tunawategemeeni sana nyinyi katika mafanikio ya michezo, nitaendelea kusema kwanini tunadhani huko kwenu tunaweza kufanikiwa zaidi, kwanza suala la utimamu wa mwili, miundombinu na uwezeshwaji ‘alisema Msitha.