Binadamu anajifunza kwa makosa-Mgunda

Kocha Mkuu wa Simba Juma Mgunda amesema makosa yaliyofanyika hadi klabu hiyo kutolewa michuano ya Ligi ya Maingwa Afrika msimu uliopita huku ikiwa imetangulia kwa kupata ushindi ugenini hayatajirudia.
Simba itacheza mchezo wa marudiano na Nyasa Big Bullets ya Malawi Septemba 18, 2022 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam baada ya kushinda kwa mabao 2-0 mchezo wa kwanza jijini Lilongwe, Malawi.
“Binadamu anajifunza kwa makosa (ilivyokuwa msimu uliopita), mechi inakwisha mpaka filimbi ya mwisho. Mechi ya kwanza Malawi ilikuwa kipindi cha kwanza, wachezaji wanatambua hilo, wapo tayari kupambana,”amesema Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda leo wakati akizungumzia mchezo huo wa marudiano.

Oktoba 21, 2021 Simba ikiwa imetangulia kwa ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi Jwaneng Galaxy ya Botswana ikikaribia kuingia hatua ya makundi ilichapwa mabao 3-1 jijini Dar es Salaam hivyo kutupwa nje ya michuano.
Amesema benchi la ufundi linatambua kwamba klabu imelipa benchi hilo malengo yake ambayo yatakiwa kufikiwa kwa pamoja na lipo tayari kuyafikia.

Naye Nahodha Msaidizi wa Simba, Mohamed Hussein amesema:”Kikubwa ni kuendelea kupambana ili tupate matokeo na kuingia kwenye hatua inayofuata. Taratibu tutakuwa tunaelekea kwenye malengo yetu.”