BurudaniMuziki

Barnaba: Albamu yangu kuvunja rekodi

MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Elias Barnabas ‘Barnaba Boy’ amesema
mauzo ya albamu yake mpya ya ‘Love Sounds Different’ inaendelea vizuri na anaamini yatavunja rekodi ya albamu zake zilizopita.

Akizungumza na gazeti la HabariLEO, msanii huyo anayemiliki studio ya kuandaa muziki ya ‘High Table Sound’, ameeleza kuwa anajivunia kuona namna mashabiki wake na Watanzania wakimuunga mkono kwa kazi ya mikono yake.

“Ukweli ninafuraha sana kuona mauzo ya albamu yangu mpya ya Love Sounds Different yapo juu, nimetembelea sehemu mbalimbali kasi inaridhisha na ninaimani inaweza kuvunja rekodi ukilinganisha na albamu zangu zilizopita,” amesema Barnabas.

Msanii huyo ameeleza kuwa ubora wa kazi alizoziandaa kwenye albamu hiyo lakini uwezo wa wasanii aliowashirikisha, anaamini ni moja ya sababu iliyochangia kazi hiyo kufanya vizuri sokoni.

Alisema mipango yake ni kwamba ikifika Desemba mwaka huu atafanya majumuisho ya mauzo ili kujua ni kiasi gani ambacho ameingiza na atawajulisha mashabiki wake ili kujua namna wanavyochangia kumpa kampeni katika kazi yake ya muziki.

Barnaba ni miongoni mwa wasanii wenye uwezo mkubwa wa kuandaa na kuimba muziki wa Bongo Fleva, ambao sasa unafanya vizuri Tanzania na nchi za jirani kama Kenya, Rwanda na Uganda.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button