Bajer, Sowah waanza kuwasha moto Misri

MISRI:HUU ndio moto wa usajili mpya! Simba imeanza kuwatisha wapinzani baada ya wachezaji wake wapya, Mohamed Bajer na Jonathan Sowah, kufungua akaunti ya mabao kila mmoja katika mchezo wa wa kimataifa wa kirafiki uliochezwa jana jioni Ismailia, Misri.
Katika mchezo huo dhidi ya Kahraba uliofanyika kwenye Uwanja wa Suez Canal Authority, nchini Misri mabao yalifungwa na wachezaji hao wapya.
Bajer, ambaye ametua Msimbazi akitokea Kenya, alifungua akaunti yake ya mabao kwa kumalizia kwa ustadi pasi safi, akidhihirisha kuwa anaweza kuwa miongoni mwa silaha hatari msimu huu.
Sowah, aliyesajiliwa kutoka Singida Black Stars, alionesha sababu ya kusakwa na vigogo baada ya msimu uliopita kutupia mabao muhimu yaliyoipeleka Singida kwenye hatua za juu za michuano ya kimataifa. Katika mchezo huu, aliongeza bao la pili.
Simba inaendelea na kambi yake nchini Misri, ikipiga mechi kadhaa za kujipima nguvu kabla ya kurejea kuanza kazi kwenye Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa, huku mashabiki wakianza kuamini moto wa Bajer na Sowah unaweza kuibeba timu kufanya vizuri zaidi msimu huu.