Baba akiri kumuua bintiye kwa risasi 4

INDIA: UCHUNGUZI wa kifo cha mcheza tenisi ngazi ya Taifa nchini India, Radhika Yadav imeeleza kwamba alipigwa risasi mara 4 mwilini mwake.
Ripoti ya uchunguzi wa mwili wa mcheza tenisi huyo ilieleza kwamba majeraha manne yamekutwa katika mwili wake na risasi zote alizopigwa zimepatikana.
Risasi tatu zilipatikana kwenye mwili wa marehemu na moja ilikutwa chini ya shingo na nyingine kwenye mgongo wa chini karibu na kiuno. Kwa jumla, majeraha manne yalipatikana kwenye mwili wa Radhika.
Babake Radhika, Deepak Yadav anadaiwa kumpiga risasi bintiye mwenye umri wa miaka 25 na kumuua katika nyumba ya ghorofa mbili ya familia hiyo katika eneo la juu la Sushant Lok siku ya Alhamisi.
Mzee huyo amekiri kosa hilo leo Ijumaa Julai 11 katika Mahakama ya Gurugram yupo chini ya ulinzi wa polisi.
Nje ya mahakama, afisa mmoja wa polisi aliwaambia waandishi wa habari kuwa wameomba mshtakiwa azuiliwe rumande kwa siku mbili. “Tunapaswa kurejesha risasi za bastola yake na kuithibitisha baada ya kutumika katika uhalifu.
Mshitakiwa huyo mwenye umri wa miaka 49, akiwa amevalia fulana na suruali, kichwani akiwa amejifunika taulo wakati akitoka kwenye gari karibu na eneo la mahakama akisindikizwa na polisi kwa ajili ya kufikishwa mahakamani.
Polisi wamesema bado wanalichunguza tukio hilo kwa umakini mno kwa pande zote za tukio ikiwa ni pamoja na kile mama wa mchezaji huyo alikuwa akifanya wakati tukio hilo likitokea.
Jana ilielezwa kwamba baba huyo alimuua bintiye kwa madai ya kuingia katika uhusiano wa kimapenzi na mwanaume asiyempenda yeye lakini leo wadadisi wa mambo wanadai kuwa Chuo cha tenisi ambacho Radhika alikuwa akifanyia mazoezi yake ndiyo kiini cha ugomvi kati ya baba na binti