Arsenal yamtolea macho Kudus

KLABU ya Arsenal imeripotiwa inafikiria uhamisho wa kiungo mshambuliaji wa Ajax ya Uholanzi Mohammed Kudus ambaye amekuwa kwenye kiwango bora katika timu hiyo ya kidachi katika siku za hivi karibuni.
Tayari Kocha Mikel Arteta amewasajili Kai Havertz, Declan Rice na Jurrien Timber majira haya ya joto na mipango ya uhamisho wa wachezaji ya Washika Mtutu hao haijafikia mwisho.
Kwa mujibu wa tovuti ya michezo football365, Arsenal huenda ikauza wachezaji kadhaa kabla ya kusajili wengine kutokana na Kanuni za Haki za Fedha.
Mkurugenzi wa Michezo wa Arsenal Edu ameripotiwa anatarajiwa kukamilisha kuwauza wachezaji kadhaa kabla ya maingizo mapya ambapo Kieran Tierney, Cedric Soares, Nicolas Pepe, Albert Lokonga, Nuno Tavares na Rob Holding wote wanaweza kuuzwa majira haya ya joto.
Nyota huyo wa kimataifa wa Ghana ana uwezo wa kucheza kiungo cha kati, kushambulia au wakati mwingine kama winga na uwezo huo umeivutia Arsenal na pia Manchester United.
Kudus mwenye umri wa miaka 22 amecheza mara 30 Ajax katika ligi kuu Uholanzi msimu uliopita akifunga magoli 11 na kutoa pasi nne za magoli.
Pia ameonesha kiwango kizuri katika Ligi ya Mabingwa Ulaya akifunga magoli manne katika michezo sita aliyocheza akiwa na miamba hiyo ya Udachi.