Arbeloa kocha mpya Real Madrid

MADRID:REAL Madrid wamemtangaza rasmi Alvaro Arbeloa kuwa kocha mpya wa kikosi cha kwanza, akichukua nafasi ya Xabi Alonso aliyeondoka kwa makubaliano ya pande zote. Arbeloa amepandishwa kutoka timu ya akiba (Castilla), hatua inayomrudisha rasmi kwenye jukwaa kubwa la klabu aliyotumikia kwa mafanikio makubwa akiwa mchezaji.
Arbeloa amekuwa kocha wa Castilla tangu Juni 2025, na kabla ya hapo alijenga jina lake ndani ya akademi ya Real Madrid tangu mwaka 2020. Safari yake ya ukocha imekuwa ndani ya klabu moja, akipita makundi mbalimbali ya vijana na kuacha alama za mafanikio. Akiwa kocha wa vijana wa chini ya miaka 19, aliiongoza timu hiyo kutwaa mataji matatu kwa msimu mmoja, pamoja na ubingwa mwingine wa ligi, jambo lililomfanya kuaminiwa zaidi na uongozi.
Kupandishwa kwake sasa kwenye kikosi cha kwanza kunakuja kama tuzo ya kazi yake ya muda mrefu ndani ya mfumo wa Real Madrid, pamoja na imani kwamba anaielewa klabu hii kuanzia mizizi hadi kileleni.
Kama mchezaji, Arbeloa alikuwa sehemu ya moja ya vipindi vya mafanikio makubwa zaidi katika historia ya Real Madrid kati ya mwaka 2009 na 2016. Aliichezea klabu mechi 238 za mashindano rasmi, akitwaa mataji makubwa ikiwemo Ligi ya Mabingwa mara mbili, Kombe la Dunia la Klabu, UEFA Super Cup, LaLiga, Copa del Rey mbili na Spanish Super Cup.
Mbali na mafanikio yake klabuni, Arbeloa pia alikuwa sehemu ya kizazi cha dhahabu cha Hispania. Aliichezea timu ya taifa mara 56, akitwaa Kombe la Dunia la 2010 pamoja na mataji mawili ya Euro ya 2008 na 2012.
Sasa anarejea Bernabeu akiwa si beki tena, bali kama kocha mkuu. Macho yote yataelekezwa kwake kuona kama ataweza kuhamisha roho ile ile ya ushindi aliyokuwa nayo uwanjani, kuja kwenye benchi la ufundi la Real Madrid.




