CHAN

Ahmed Ally: Taifa Stars Siyo yatima

tuijaze Benjamin Mkapa

DAR ES SALAAM: MSEMAJI wa Klabu ya Simba SC na mhamasishaji wa Taifa Stars Ahmed Ally, amewataka Watanzania kuelekea mechi ya ufunguzi ya michuano ya CHAN 2024, kuweka uzalendo kwa kuiunga mkono Taifa Stars.

Ahmed, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha mashabiki wa soka nchini, amesema kuwa Tanzania haina sababu ya kushindwa kujaza mashabiki 60,000 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya kwanza ya mashindano hayo makubwa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani.

“Tuna watu zaidi ya milioni sitini, tukishindwa kutoa watu elfu sitini tu siku ya mechi ya kwanza ya Taifa Stars, tutakuwa hatujatenda haki. Timu ya taifa si yatima, iko kwenye ardhi yake, inahitaji sapoti yetu kwa vitendo,” alisema Ahmed Ally Dar es Salaam leo wakati akizungumza na mashabiki wa Kawe.

Ahmed amewaomba Watanzania kuacha shughuli zao kwa siku hiyo muhimu na kuungana kwa pamoja uwanjani.

“Hakuna uzalendo wa kweli bila matendo. Kuanzia tarehe mbili Agosti, uzalendo wetu utaonekana kwa namna tunavyojitokeza kwa wingi uwanjani. Tuwaoneshe wachezaji wetu kuwa wako nyumbani, na siyo wageni,” alisema Ahmed.

Ahmed pia amesisitiza kuwa mechi ya kwanza ndiyo inatoa dira ya mashindano yote, na kama taifa mwenyeji, ni lazima Tanzania ioneshe mfano bora wa mapokezi, maandalizi na ushiriki wa mashabiki.

Ili kuongeza mvuto na mshikamano, Ahmed amewataka mashabiki kuvaa jezi za Taifa Stars za buluu au kijani siku ya mechi hiyo huku akiamini kuwa nguvu ya mashabiki ndiyo silaha kubwa inayoweza kuwasaidia wachezaji wa Taifa Stars kujiamini na kupambana kwa nguvu zaidi.

Related Articles

Back to top button