Ligi Kuu

Ahemd Ally: Nangu ataangamiza wengi

DAR ES SALAAM: MSEMAJI wa Klabu ya Simba SC, Ahmed Ally, amesifu kiwango kikubwa kilichooneshwa na mshambuliaji wa timu hiyo, Wilson Nangu, akisema atakuwa tishio na kuwaangamiza wengi.

Akizungumza Dar es Salaam, msemaji huyo alisema klabu hiyo iliona thamani yake mapema na ndiyo maana iliamua kupambana kuhakikisha inampata wakati wa dirisha la usajili.

Ahmed amesema Nangu ameanza kuonesha kile ambacho Simba walikiamini juu yake, hasa baada ya kufunga bao muhimu la kusawazisha wakati timu hiyo ikiwa nyuma kwa 1-0, dhidi ya JKT Tanzania jambo lililobadilisha mwelekeo wa mchezo na kutoa morali kwa wachezaji na mashabiki, kabla ya Simba kukamilisha ushindi wa mabao 2-1 mwishoni mwa wiki.

“Tuliona kipaji cha Wilson Nangu, tuliamini atakuja kuisaidia Simba. Kila mmoja ameona kwanini tuling’ang’ana kumchukua. Ataendelea kuwaangamiza watu wengi zaidi. Sasa anacheza mpira wa kiufundi, mpira wa kitalaam,” amesema Ahmed.

Hili linakuwa bao lake la pili mfululizo, baada ya kutikisa nyavu pia kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, jambo linaloashiria mabadiliko ya aina ya uchezaji wake.

Akifafanua zaidi, Ahmed amesema kiwango cha Nangu ni matokeo ya kazi kubwa inayofanyika katika uwanja wa mazoezi, chini ya benchi la ufundi.

“Ni mambo wanayofundishwa wachezaji uwanjani katika mazoezi. Huu ni mpango unaotengenezwa kwenye uwanja, na Nangu ni mfano wa mchezaji anayetekeleza maelekezo,” ameongeza.

Related Articles

Back to top button