Aaron Taylor-Johnson kuwa James Bond mpya?

LONDON: Muigizaji kutoka Uingereza, Aaron Taylor-Johnson, ametia saini kuwa balozi wa kimataifa wa kampuni ya saa za kifahari Omega,hatua inayozua maswali kuhusu nafasi yake kama James Bond mpya. Omega ni mshirika rasmi wa safu ya filamu za James Bond, na hatua hiyo imechochea uvumi kwamba huenda Aaron ndiye atakayemrithi Daniel Craig katika nafasi hiyo maarufu.
Je, utambulisho mpya wa James Bond umevuja kwa bahati mbaya au la?
Tangazo hilo jipya kutoka Omega limeibua maswali mengi mitandaoni. Kutokana na uhusiano wa karibu wa kampuni hiyo na franchise ya 007, wengi wanahisi kuna dalili kwamba Aaron Taylor-Johnson anaweza kuwa ndiye James Bond ajaye.
Aaron alitangazwa hivi karibuni kuwa balozi mpya wa Omega, na picha zake akiwa ofisini kwao huko Bienne, Uswisi—makao makuu ya utengenezaji wa saa hizo zimesambazwa sana.
Katika taarifa rasmi, Omega ilisema:
“Omega inamkaribisha Aaron Taylor-Johnson kwenye nyumba yetu ya kutengeneza saa huko Bienne. Muigizaji na mshindi wa Golden Globe aliingia katika nyumba yetu ya utengenezaji wa saa kwa ziara ya kipekee, akikutana na watengeneza saa zetu.”
Japo hakuna uthibitisho rasmi kutoka kwa watayarishaji wa filamu za Bond, hatua hii imeacha mashabiki wakiwa na maswali mengi kuhusu hatma ya ajenti 007.