Majiha apima afya kutetea ubingwa wa WBC Afrika Mbeya

DAR ES SALAAM: BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Fadhili Majiha amekamlisha zoezi la kupima afya kwa pambano la kutetea mkanda wa ubingwa wa WBC Afrika dhidi ya Sabelo Ngebiyana wa Afrika Kusini.
Majiha amekamilisha vipimo chini ya Daktari wa Kamisheni ya Kusimamia ngumi za Kulipwa nchini, TPBRC, Dkt Hadija Hamisi, tayari kwa kupanda ulingoni Julai 20, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mbeya Pub, Jijini Mbeya.
Majiha atapanda ulingoni hapo kutetea mkanda wake wa ubingwa wa WBC Afrika katika pambano hilo ambalo limeandaliwa na Promosheni ya Kemmon Sports Agency chini ya Saada Salum.
Akizungumza na Spotileo leo, Majiha alisema anamshukuru Mungu anaendelea vizuri na maandalizi kabla ya kesho kuingia jijini Mbeya kuendelea na maandalizi yake ya mwisho.
“Nashukuru Mungu naendelea vizuri na maandalizi yangu, leo nimekamilisha vipimo vya Afya, kesho nategemea nitakuwa Mbeya kuendelea na maandalizi ya mwisho.
Sabelo ameshakuja siyo mgeni lakini naamini hajapigwa kama nitakavyompiga kwa sababu aliocheza nao hawakuweza kumpiga vizuri,” anasema Bondia huyo.
Kwa upande wa daktari wa Kamisheni ya Kusimamia Ngumi za Kulipwa nchini, TPBRC, Dkt Hadija Hamisi amefunguka kuwa wamekamilisha zoezi la hilo kisheria kwa mabondia wote wanaotarajia kupanda ulingoni katika pambano hilo kwa lengo la kulinda afya zao.
Ikumbukwe, Majiha alishinda mkanda wa ubingwa huo mwaka jana kwa kumchapa kwa pointi Bongani Mahlangu kutoka Afrika Kusini.




