Ligi Daraja La Kwanza

Simba yamuweka sokoni Inonga

DAR ES SALAAM: UONGOZI wa Simba umeweka wazi bado hawajapokea ofa kutoka timu yoyote inayohitaji kumsajili beki wao Henock Inonga.

Imedaiwa kuwa kuna ofa mbili kutoka FAR Rabat FC ya Morocco na FC Metz ya nchini Ufaransa ambayo hivi karibuni kulisambaa picha ya Inonga akionekana akiwa na jezi za timu hiyo ndipo SpotiLeo ikaamua kuutafuta ukweli wa jambo hilo.

Taarifa zilizopatikana ni kuwa uongozi wa Simba wapo kwenye mipango ya kumuuza beki huyo kwa lengo la kuendelea kufanya maboresho ya kikosi cha timu hiyo kwa msimu ujao.

“Inonga ameshaondolewa kwenye mipango ya kikosi kwa msimu ujao, milango ipo wazi kwa timu inayohitaji beki huyo kwa sababu Simba wanataka kufanya maboresho makubwa ndani ya kikosi cha timu hiyo,” amesema.

Akizungumza na Spotileo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema hakuna ofa waliyopokea na milango ipo wazi kwa timu itakayohitaji huduma ya Inonga.

Amesema Inonga ni mchezaji wa Simba hadi mwakani ila wapo tayari kumuuza endapo klabu au timu itapeleka ofa mezani kumpata beki huyo.

“Hatuwezi kuzuia mchezaji kama kuna ofa itakuja mezani kwetu, kikubwa tunaangalia maslahi kwa pande zote klabu hata kwa mchezaji husika, anapotoka mtu basi ataletwa mtu bora zaidi,” amesema meneja huyo.

Related Articles

Back to top button