Ligi KuuNyumbani

Mbeya City kutorudia makosa

KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Abdallah Mubiru, amesema kuwa hawatarudia makosa yaliyosababisha wakapoteza mchezo uliopita dhidi ya Singida Big Stars, watakaposhuka kuikabili Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya Septemba 9.

Mbeya City wanaoshika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi tatu baada ya kushuka uwanjani mara mbili, watakuwa na kazi ya ziada kuwakabili Prisons wanaoshika nafasi ya tisa wakiwa na pointi tatu.

Akizungumza na gazeti la HabariLEO, Mubiru amesema Singida Big Stars, waliwaonesha mapungufu yao ambayo wameyafanyia kazi katika mapumziko ya ligi hivyo hawatarajii kurudia makosa ingawa anaamini itakuwa mechi ngumu kutokana na historia ya timu hizo mbili.

“Najua utakuwa mchezo mzuri lakini wenye maana kubwa kwetu, tunatakiwa kushinda ili kurejesha hali ya kujiamini kikosini baada ya morali yetu kushuka tulipopoteza mechi iliyopita tunarudi nyumbani ili tuweze kukusanya pointi tatu kwenye mchezo ulio mbele yetu,” amesema Mubiru.

Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Patrick Odhiambo.

Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Patrick Odhiambo, amesema anaingia kwenye mchezo dhidi ya Mbey City kwa tahadhari kubwa lakini malengo ni kupata ushindi na kukusanya pointi tatu japokuwa anaamini halitakuwa jambo jepesi.

“Kila timu inaingia kwenye mchezo kutafuta pointi tatu, naamini utakuwa mchezo mgumu
kutokana na historia iliyopo lakini tunaingia kwenye mechi hii tukiwa na lengo moja ambalo
ni pointi tatu, naamini vijana wangu wataenda kupambana na kuhakikisha tunafanikisha malengo yetu,” amesema Odhiambo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button