BurudaniFilamu

HONEST THIEF: Mapenzi yana nguvu ya kuweza kuhamisha mlima

JE! Umewahi kujiuliza itakuwaje pale jambazi sugu kwenye benki mbalimbali anayetafutwa
na vyombo vya dola bila kupatikana anapoamua kukiri na kujisalimisha, nini kitatokea?

Ndiyo, amejitolea sehemu kubwa ya maisha yake kuiba katika benki mbalimbali, ameshaiba zaidi ya dola milioni 9, fedha taslimu, wakati alipokuwa jambazi sugu. Lakini si kwamba kila mtu anajua kwamba yeye ni mwizi wa fedha hizo.

Pamoja na yote, huyu ni mwizi aliyekubuhu ambaye amepewa jina la utani la “Jambazi wa Ndani na Nje” kutokana na kutumia akili nyingi sana katika kuiba fedha nyingi. Ingawa analichukia jina la “Jambazi wa Ndani na Nje” lakini hakuna namna.

Kwa sababu anakutana na mpenzi wa maisha yake, mwanadada Annie Wilkins. Huyu ni Tom Dolan ambaye anabadilika kabisa kutoka kiumbe hatari anayeogopwa na kuwa kiumbe kipya baada ya kukutana na Annie, mhitimu wa somo la saikolojia anayefanya kazi katika
kitengo cha uhifadhi.

Baada ya kumpata Annie, sasa anadhani kuwa yuko tayari kujisalimisha ili awe safi; kujisalimisha huko si tu kwa Annie, bali kwa vyombo vya dola pia. Maana uhusiano mwema hauwezi kujengwa kwa uongo. Unaona!

Hakuwahi hata kufikiria kama angeweza kukutana na mtu ambaye anaweza kumfanya atulie. Anaona kuwa inapaswa kuwa jambo rahisi tu. Kupiga simu katika taasisi ya FBI na kukiri makosa.

Kwa hivyo, anaamua kufanya hivyo kwa matarajio ya kwamba atapewa hukumu ya kifungo chepesi ili aweze kuachana na historia yake ya uhalifu. Mara ya kwanza, FBI hawamwamini kabisa. Wanadhani anawafanyia dhihaka.

Hata hivyo, mpelelezi Sam Baker anawatuma wasaidizi wake wawili: John Nivens na Ramon Hall kumhoji na baadaye Tom anawapeleka kwenye kitengo cha uhifadhi ambapo fedha zake zimefichwa, huko wanakuta dola milioni 3.

Hali ya hewa inabadilika, wapelelezi Niven na Hall hawatendi sawasawa na maadili yao. Badala ya kutimiza majukumu yao, wao wanataka kuzichukua fedha hizo na kumtupa Tom
gerezani.

Na wanapanga kufanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba Tom anafungwa gerezani maisha yake yote. Nivens na Hall wanamkabili Tom katika hoteli yake wakiwa na bastola, lakini Baker anawasili hapo bila kutarajiwa; Nivens anamuua Baker, na Tom analazimika kukimbia na Annie mara tu anapofika hotelini.

Tom anamwambia Annie kila kitu na anamtaka atoroke, akihofia usalama wake. Hata hivyo, Annie anarudi kwanza kazini kwake kwenye kitengo cha uhifadhi ili kupata ushahidi wa kamera ya usalama inayowaonesha Nivens na Hall wakiiba fedha za Tom.

Nivens na Hall wanajitokeza na Nivens anampiga Annie, karibu amuue. Kwa kulipiza kisasi, Annie anamchoma Nivens mguuni na mkasi na anajaribu kutoroka lakini Nivens anamzimisha.

Hall anamfanyia Nivens ghilba akifikiri Annie amekufa na anauchukua ushahidi, bila Nivens kujua. Tom anamkuta Annie akiwa amepoteza fahamu na kumkimbiza hospitalini.

Halafu anatoroka kwa sababu polisi wanataka kumkamata, katika harakati hizo anamshinda mshirika  wa Baker, Sean Meyers katika mapambano ya ngumi, na kumwambia kuhusu
kile kilichotokea kabla ya kutoroka. Sasa Nivens anapanga njama za kumuua Annie.

Anaenda hospitalini lakini anashindwa kumfikia kwa sababu yuko chini ya ulinzi wa polisi.
Tom anamvizia Hall nyumbani kwake na kumshawishi aachilie video za usalama alizozipata  katika kitengo cha uhifadhi ambazo zitasaidia katika ushahidi wa eneo la nyumba ambalo
fedha zilihifadhiwa.

Kisha Tom anamtoa Annie kutoka hospitalini na kumwacha mahali salama, kisha anaiharibu nyumba ya Nivens. Nivens anakimbilia kwenye nyumba salama na kukutana na Hall,
ambapo Tom anakabiliana nao.

Nivens anapogundua kuwa Hall amechukua video za usalama, anamuua kwa hasira, kisha anamjeruhi Tom, na kutoroka. Akitarajia jambo hilo, Tom anapandikiza bomu kwenye gari la Nivens, na kumlazimisha aite kikosi maalumu cha kutegua mabomu ili kulitegua.

Polisi wanapogundua kuhusu fedha zilizoibiwa, Nivens anakamatwa. Mpelelezi Sean Meyers
anapokea kinasa sauti ambacho kilirekodi mazungumzo kati ya Nivens na Hall kabla ya mapambano ya silaha kwenye nyumba salama, sauti inayothibitisha kuwa Tom hana hatia
kwa kifo cha Baker.

Kisha Tom anajisalimisha mwenyewe kwenye mamlaka, na Meyers anaahidi kumtetea Tom ili apatiwe hukumu nyepesi. Filamu ya Honest Thief (Mwizi Mwaminifu)inaonesha kwamba Tom anamaanisha kwa vitendo anaposema kuwa anataka kujisafisha.

Ndiyo, anampata anayempenda na kuamua kuwa mtu wa familia anayejaribu sana kurekebisha makosa yake ya zamani na kuanza maisha mapya. Lakini tatizo linakuja
pale filamu hii, badala ya kuonesha suluhisho inaonesha mwisho unaoshangaza kidogo.

Hakuna suluhisho halisi, ni mfululizo tu wa matukio yasiyowezekana ambayo yanaacha maswali. Filamu hii ya dakika 99 imetoka rasmi Oktoba 16, 2020 nchini Marekani, na
imefanikiwa kuingiza dola milioni 29.4 kupitia maonesho ya sinema.

Related Articles

Back to top button