Slot akaribia ukocha Spurs
ARNE Slot atakuwa kocha mpya wa Tottenham Hotspur iwapo wakala wake Rafaela Pimenta ataweza kujadiliana kuvunja mkataba wake katika klabu ya Feyenoord Mei 24.
Mdachi huyo ni chaguo namba moja la mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy lakini hakuna kinachoweza kuthibitishwa hadi Pimenta amekutana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Feyenoord, Dennis te Kloese jijini Rotterdam.
Slot ana kipengele cha kutolewa cha pauni milioni tano sawa na shilingi bilioni 14.5 katika mkataba wake lakini ni vigumu kuuamilisha hadi majira ya yajayo ya joto.
Fenenoord ambayo imetwaa ubingwa wa Uholanzi hivi karibuni haitaki kumwachia Slot na huenda makubaliano yakafikiwa iwapo Tottenham itaheshimu na kulipa fidia ya zaidi ya pauni milioni 10 sawa na shilingi bilioni 29.
Slot anatarajiwa kuhama pamoja na msaidizi wake Marino Pušić kwenda England na Spurs inaungana na Liverpool kumwania kiungo wa Feyenoord Orcun Kökcü anayekadiriwa kuwa na thamani ya pauni milioni 40 sawa na shilingi bilioni 116 ambaye Slot ataka awe mchezaji wa kwanza kumsajili Tottenham.




