
COASTAL Union licha ya kuwa kwenye hali mbaya msimu huu wanaamini watasalia kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu ujao.
Coastal inashika nafasi ya 13 ikiwa na pointi 26 baada ya michezo 25, ikitofautiana kwa pointi saba na Polisi Tanzania inayoburuza mkia, pointi sita dhidi ya Ruvu Shooting iliyopo nafasi ya 15 huku ikiwa sawa kwa pointi na Tanzania Prisons inayoshikilia nafasi ya 14.
Ofisa Habari wa Coastal, Jonathan Tito ameliambia gazeti la HabariLEO kwamba wanaamini
wamekuwa kwenye hali mbaya kutokana na ugumu wa ligi ya msimu huu lakini pia wamejipanga kuhakikisha wanapata matokeo kwenye mechi tano zilizosalia kabla pazia halijafungwa.
“Unajua hii michezo ya mwishoni ndiyo imetukwamisha, tulipanga kuhakikisha tunapata matokeo mazuri lakini ndiyo hivyo wapinzani nao wameonesha ugumu wao, ligi imekuwa ngumu msimu huu, kila timu inataka kufanya vizuri.
“Lakini tunaamini tutasalia kwenye ligi msimu ujao, hatuna hofu kuhusiana na hilo, tunapambana, tunajipanga, tunaweka sawa kikosi kuhakikisha hatupotezi mchezo kwenye mechi zilizobaki na tunaamini msimu ujao tutaendelea kuwepo,” amesema Tito.
Timu hiyo ya jijini Tanga ambayo imeshinda mechi mbili, sare mbili na kufungwa mmoja kwenye mechi tano zilizopita, mechi tano zinazokuja itaumana na Dodoma Jiji, Mtibwa Sugar, Ihefu, Azam na Simba.