ADEL AMROUCHE: Kocha Stars aliyebeba matumaini ya Watanzania

WIKI hii Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Pindi Chana alimtambulisha rasmi Adel Amrouche kuwa Kocha Mkuu wa timu ya taifa, ‘Taifa Stars’.
Adel Amrouche baada ya kutambulishwa alizungumza na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza akiahidi kuwanoa wachezaji vyema ili kuiweka juu zaidi Tanzania katika ulimwengu wa soka, huku akisisitiza ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali katika kufanikisha kazi
yake.
Taifa Stars kwa sasa ipo kwenye kampeni za kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2023 na Machi 24 inatarajiwa kucheza dhidi ya Uganda Cranes katika Uwanja wa Suez Canal nchini Misri na watarudiana Machi 28 mwaka huu, Dar es Salaam.

Amrouche raia wa Ubelgiji mwenye asili ya Algeria anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Kim Poulsen aliyeshushwa kwenye timu za vijana mwishoni mwa mwaka jana baada ya kocha
huyo raia wa Denmark kushindwa na Uganda katika mechi ya kufuzu kwa michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani (Chan).
Amrouche atahitaji zaidi bahati kwani kusema kuwa atakuwa ameiandaa timu hilo si kweli lakini mwenyewe ameweka wazi anahitaji ushirikiano kutoka kwa wadau na sapoti ya
mashabiki.
“Muhimu zaidi katika kazi hii ni mashabiki wetu kwa sababu hili ndilo jambo la kwanza lililonisukuma kuja hapa,” alisema na kuongeza: “Katika uzoefu wangu wa miaka 21 kufundisha soka Afrika, nadhani ni Congo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) pekee
na Algeria kidogo ndio nimeona sapoti kama ya Tanzania.
Wanapokuwa pamoja, hawaweki tu presha kwa mpinzani bali huwapa motisha wachezaji pia, nawaomba waje kuisapoti timu yao ya taifa,” alisema.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 54 ataanza katika hatua hiyo ambayo ilimwondoa Kim Poulsen dhidi ya Uganda Cranes watakapokutana mara mbili baadaye mwezi huu katika mechi za kufuzu Afcon, Kundi F.
Kwa imani ambayo Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan imeonesha kwa
Amrouche kuwa ni kocha bora na atakayekuza soka la Tanzania kulingana na wasifu wake, huku ikisema watamlipa mshahara, Watanzania wanatarajia kupata furaha.
Tatizo litabaki kwa wachezaji watakaopewa dhamana ya kuipeperusha bendera ya Taifa je,
wataweka utaifa mbele na kucheza kufa au kupona ili timu ifanye vizuri ndani na nje ya nchi?
Kigezo cha kuwa Kocha Bora wa Afrika Mashariki mwaka 2013 wakati akiinoa na kuipa Kenya, Harambee Stars ubingwa wa Cecafa Challenge na kabla na kufika nusu fainali mara mbili akiwa na Burundi anahitaji zaidi wachezaji kuonesha uwezo wao na kupambana hadi tone la mwisho.
Ile rekodi yake ya kucheza michezo 20 bila kufungwa akiwa na Harambee Stars inawezekana kujirudia akiwa na Taifa Stars ikiwa wachezaji wataonesha kiwango bora maana wanalipwa vizuri na kwa wakati chini ya udhamini wa Bia ya Serengeti.
Kingine cha kujivunia Amrouche ambaye ni mkufunzi wa walimu mwenye Pro Licence wa Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) anazungumza lugha ya Kiswahili hivyo hakuna ugumu wa
kuwasiliana na wachezaji.
Mara nyingi Taifa Stars ilipokuwa inafundishwa na makocha ambao si wazawa na hawajui Kiswahili mashabiki walijenga dhana kuwa hawamwelewi kocha kwa sababu ya lugha, lakini kwa Amrouche hilo la lugha halipo kabisa.Hakuna suala la lugha gongana.
Kwa Amrouche, Taifa Stars imepata ‘combo’ maana ni kocha mkufunzi na ana Shahada ya Uzamili katika kuwasoma watu na Utimamu, hivyo pamoja na kuwa atakuwa na wasaidizi wa Physio na Fitness lakini yeye mwenyewe ana uwezo wa kung’amua mchezaji fulani ana tatizo kwenye utimamu.
Tanzania na Uganda zote zina pointi moja katika msimamo kwenye mechi mbili huku Algeria ikiongoza kwa pointi sita na Niger ikiwa na pointi mbili kwenye michezo miwili.
Taifa Stars ilifungwa nyumbani na Algeria 2-0 na ikatoka sare ya 1-1 na Niger ugenini pia Algeria waliifunga Uganda 2-0 na Uganda ikatoka sare ya 1-1 na Niger nyumbani.
Kwa kuonesha mchezo huo ni muhimu tayari Kocha Mkuu wa Uganda, The Cranes amemrejesha Steven Mukwala kwa ajili ya mechi hizo za kufuzu fainali za Kombe la Mataifa
ya Afrika.
Mukwala, mchezaji wa zamani wa URA ambaye kwa sasa anachezea Asante Kotoko ya Ghana aliichezea timu hiyo mara ya mwisho Novemba 14, 2021 akiingia dakika ya 70
kuchukua nafasi ya Martin Kizza katika kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Mali katika mechi ya
kufuzu kwa Kombe la Dunia la Fifa 2022.