Muziki

Linah amjibu Zuchu amwombea kipaji cha milele

DAR ES SALAAM: MSANII wa Bongo Fleva, Linah Sanga, amemjibu mwanamuziki Zuchu kwa ujumbe mzito wenye maneno ya maonyo, ushauri na kejeli, huku akimtakia kila la heri katika safari yake ya muziki wa milele.

Kupitia ujumbe aliouandika, Linah amesema amesikitishwa na kauli za Zuchu kiasi cha kujiuliza kama amekuwa mtu aliyesahaulika katika tasnia ya muziki, licha ya mchango alioutoa kwa miaka mingi.

“Mdogo wangu Zuchu, nimekaa nimetafakari labda mimi ni mfu ninayetembea na sijui… nimeumia sana kama dada yako! Kwenye hii tasnia nina mchango mkubwa sana, na ukumbuke kwenye maisha kuna kupanda na kushuka,” aliandika Linah.

Ameongeza kuwa maisha ya ustaa ameyaishi kwa muda mrefu na anaamini alikuwa miongoni mwa wasanii waliofungua njia kwa vijana wengi wa kike kuingia kwenye muziki wa Bongo Fleva.

Linah amemtaka Zuchu kujifunza kuheshimu wengine, kumcha Mungu na kutambua kuwa teknolojia haiwezi kusahau mambo yaliyowahi kutokea.

“Siwezi kukuombea mabaya ila nitakushauri kama dada, ogopa Mungu na technology huwa havisahau. Nakutakia kila la kheri kwenye muziki wako,” aliandika.

Hata hivyo, sehemu iliyozua hisia zaidi ni pale Linah alipomalizia ujumbe wake kwa maneno ya kejeli akisema:

“Nakuombea kipaji Cha milele uje kutumbuimbia huku kuzimu.”

Katika ujumbe huo huo, Linah ameongeza kauli nyingine yenye utata akisema: “Kuna mwenye mke mwenza halafu kuna mwenye wake wenza a.k.a kijiji”

Urafiki wa Zamani Lina na diamond

Jambo jingine linalofanya majibu ya Linah yazungumzwe zaidi ni historia yake ya ukaribu na mwanamuziki Diamond Platnumz.

Linah Sanga aliwahi kuwa na urafiki wa karibu na Diamond Platnumz miaka mingi iliyopita, wakati ambapo wawili hao walikuwa bado wanajenga majina yao katika tasnia ya muziki.

Picha yao ya zamani inayosambaa inaelezwa kuwa ilipigwa takribani miaka 17 iliyopita, kipindi ambacho urafiki wao ulikuwa umekolea.

Historia hiyo inakumbusha kuwa Linah si mgeni katika mazingira ya tasnia ya muziki wa Bongo Fleva, jambo linalomfanya ujumbe wake kwa Zuchu kuvuta hisia na mijadala miongoni mwa mashabiki.

Related Articles

Back to top button