Zuchu amlipua Linah

DAR ES SALAAM: MSANII wa Bongo Fleva, Zuhura Othumani ‘Zuchu’, amemhusisha mwanamuziki mkongwe Linah Sanga katika mvutano wake na Nandy, baada ya kumjibu Linah kwa maneno makali yaliyofuatia maoni yake kuhusu ujio wa albamu mpya ya Nandy.
Sakata hilo limeibuka baada ya Linah Sanga kuandika ujumbe akieleza kuwa anaisubiri kwa hamu albamu mpya ya Nandy, akisema haiwezi kutoka mapema vya kutosha kwani anatamani ianze kuisikiliza na kuifurahia.

Hata hivyo, ujumbe huo haukupita kimya kwa Zuchu, ambaye aliamua kutoa maoni yake kwa kumjibu Linah kwa maneno yaliyovuta hisia za mashabiki.
Katika ujumbe wake, Zuchu aliandika: “Na ninavyokuheshimu nikuache tu, ndege mnana. Na watu mana kutoka kuwa mke mwenza mpaka msanii wake na jeuri hiyo huna.”
Kauli hiyo imezua mjadala kuhusu uhusiano wa Zuchu, Linah na Nandy, huku baadhi ya mashabiki wakisubiri kuona kama mvutano huo utaendelea.




