Michezo Mingine

Gukesh, Sindarov kupambania taji la dunia la chess

USWISI: BINGWA mtetezi wa dunia wa mchezo wa chess, D Gukesh kutoka India, anatarajiwa kukutana na Javokhir Sindarov wa Uzbekistan katika pambano la kuwania taji la dunia litakalochezwa kwa mfumo wa michezo 14 ya classical chess mjini Cologny, nje kidogo ya Geneva, Uswisi.

Wachezaji hao wawili wana jumla ya umri wa miaka 40, jambo linaloonesha ujana wa washindani wanaowania heshima kubwa katika mchezo huo.

Gukesh anaingia katika pambano hilo akiwa na changamoto ya kurejesha kiwango chake baada ya kushuka kwa nafasi na alama katika viwango vya kimataifa.

Kwa upande wake, Sindarov amekuwa katika kiwango bora, akipanda hadi nafasi tano za juu duniani. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Sindarov anamzidi Gukesh kwa alama 72, hali inayoongeza mvuto wa pambano hilo.

Wachezaji hao waliwasili Cologny siku chache kabla ya kuanza kwa mashindano na kufanya maandalizi ya mwisho katika Fondation Martin Bodmer, maktaba na makumbusho yenye vitabu na maandishi adimu.

Gukesh, ambaye ataanza mchezo wa kwanza akiwa na rangi nyeusi, ana uzoefu wa kushiriki pambano la kuwania ubingwa wa dunia baada ya kumshinda Ding Liren mwaka 2024.

Katika mahojiano yaliyochapishwa na Chess.com, Gukesh alikiri kuwa amekuwa na wakati mgumu kukabiliana na matarajio na shinikizo. Alisema baadhi ya matokeo yake mabaya ya hivi karibuni hayakutokana na udhaifu wa kiufundi pekee, bali pia matarajio makubwa yaliyokuwa yakimzunguka.

Alitolea mfano mashindano ya Chennai Grand Masters, ambako alikosa kutumia vizuri nafasi ambazo kwa kawaida angeweza kuzishinda.

Hata hivyo, Gukesh ana kumbukumbu ya ushindi muhimu dhidi ya Ding Liren mwaka 2024, aliposhinda kwa pointi 7.5 dhidi ya 6.5 baada ya kupoteza mchezo wa kwanza. Katika pambano hilo alionesha uimara wa kisaikolojia kwa kuendelea kupambana na kukataa baadhi ya nafasi za sare.

Uzoefu huo unaweza kuwa muhimu katika kukabiliana na Sindarov, ambaye anaingia kwenye pambano hili akiwa na mwenendo mzuri wa matokeo.

Kwa upande wa Sindarov, nafasi ya kupambana na bingwa mtetezi ni fursa ya kuthibitisha uwezo wake katika jukwaa kubwa zaidi la chess duniani.

Hata hivyo, ushindi hautategemea viwango pekee, bali pia maandalizi, mikakati na uwezo wa kuhimili shinikizo katika michezo yote 14. Hivyo, pambano hilo linawakutanisha Gukesh mwenye uzoefu wa kutetea taji na Sindarov mwenye kiwango bora cha sasa katika vita ya kuwania ufalme wa chess duniani.

Related Articles

Back to top button