Fadlu aweka wazi hali ya majeruhi Yanga

DAR ES SALAAM: KOCHA wa Yanga, Fadlu Davids, amesema kikosi chake kinahitaji wiki moja ya maandalizi ya pamoja ili kuimarisha utimamu wa wachezaji na kuongeza ubora wa uchezaji kabla ya kukutana na MC Alger katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Fadlu amesema baadhi ya wachezaji wa kimataifa walirejea kutoka kwenye majukumu ya timu zao za taifa wakiwa wamechoka kutokana na safari ndefu na kucheza dakika nyingi katika michezo miwili iliyopita, hali iliyomlazimu kuwapumzisha baadhi yao katika mchezo wa Ijumaa na kuwatumia wengine kipindi cha pili.
Akizungumza na waandishi wa Habari Dar es Salaam leo mesema pamoja na muda mfupi wa maandalizi, tayari ameanza kuona hatua za maendeleo katika utekelezaji wa mfumo anaoutaka, akibainisha kuwa timu haiwezi kufikia ukamilifu baada ya wiki moja tu ya mazoezi.
Kocha huyo ameeleza kuwa wachezaji Max Nzengeli na Pacome Zouzoua bado wanasumbuliwa na majeraha ya muda mrefu, huku Yao Attohoula, Duke Abuya, Clement Mzize na Dickson Job wakiwa miongoni mwa waliorejea baada ya kukaa nje kwa muda kutokana na majeraha, lakini bado wanahitaji kurejesha utimamu wao wa kimwili.
Ameongeza kuwa Mudathir Yahya naye alikosa wiki tatu za mazoezi kutokana na adhabu ya kadi nyekundu, hivyo wiki nzima ya maandalizi akiwa na kikosi kizima itasaidia kuongeza utayari wa wachezaji hao kuelekea mchezo dhidi ya MC Alger.
Akizungumzia kiwango cha Stephane Aziz Ki na Clement Mzize, amesema wachezaji hao tayari wanajulikana kwa uwezo wao na jukumu lake ni kuhakikisha anawapa nafasi na uhuru wa kuonesha vipaji vyao ndani ya mfumo wa timu.
Amesema ameanza kuona maboresho katika uchezaji wao, lakini bado anaamini wana uwezo mkubwa zaidi wa kuisaidia Yanga watakapofikia kiwango chao cha juu.
“Wachezaji hawa hawahitaji kuthibitisha kwa Watanzania jinsi walivyo wazuri. Kila mmoja anajua ni wachezaji bora. Ni jukumu langu kuwaweka katika nafasi ambazo watakuwa huru kuonesha uwezo wao na kutumia vipaji vyao kuisaidia timu. Wakicheza katika kiwango chao cha juu, hawatazuilika,” amesema Fadlu.
Kocha huyo amesisitiza kuwa anajitathmini kwanza kabla ya kuikosoa timu, akiamini Yanga itaendelea kuboresha kiwango chake kadiri maandalizi yanavyoendelea ili kufikia kiwango kinachotakiwa katika mashindano ya Afrika.




