Afcon 2027 kupigwa katika viwanja sita, Tanzania yatoa vitatu

NAIROBI: SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limetangaza viwanja sita vitakavyotumika kuandaa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027, itakayofanyika kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda.
Uamuzi huo umetangazwa katika mkutano wa CAF uliofanyika nchini Nigeria mwishoni mwa wiki, huku nchi hizo tatu za Afrika Mashariki zikijiandaa kuandaa mashindano hayo makubwa kwa mara ya kwanza kwa ushirikiano wa mataifa matatu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tanzania imepata nafasi ya kutumia viwanja vitatu vilivyopo Arusha, Dar es Salaam na Zanzibar, hivyo kuwa na idadi kubwa zaidi ya viwanja kati ya mataifa matatu mwenyeji.
Kenya itatumia Uwanja mpya wa Talanta jijini Nairobi wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000, ambao unatarajiwa kufunguliwa Januari 2027.
Kwa upande wa Uganda, mechi zitachezwa katika Uwanja wa Mandela jijini Kampala pamoja na Uwanja mpya wa Hoima City uliopo Hoima.
Hata hivyo, CAF bado haijatangaza uwanja utakaotumika kuandaa mchezo wa fainali ya mashindano hayo yatakayoshirikisha timu 24 za taifa.
AFCON 2027 imepangwa kuanza Juni 19 hadi Julai 17, 2027, huku mataifa mwenyeji yakitarajiwa kutumia fursa hiyo kukuza soka, utalii na uchumi wa Afrika Mashariki.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuwa ya kihistoria kutokana na kufanyika katika mataifa matatu, jambo litakaloiweka Afrika Mashariki katika ramani ya soka la kimataifa.




