Nyumbani

Yanga, JKT Queens watambiana

DAR ES SALAAM: KOCHA wa Yanga Princess, Saidi Maulid, amesema kikosi chake kimejiandaa kwa nidhamu ya mbinu kukabiliana na JKT Queens katika mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa KMC kesho Dar es Salaam.

Maulid amesema Dar es Salaam leo kuwa JKT Queens ni timu yenye uzoefu mkubwa, ikiwa imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake mara nne, Kombe la Jamii mara mbili na ubingwa wa CECAFA mara mbili, hivyo wanatambua ukubwa wa changamoto inayowakabili.

“Tunajua mchezo utakuwa mgumu kwa sababu tunakutana na timu nzuri yenye uzoefu mkubwa wa ligi. Tunaichukulia kwa uzito na tunahitaji kuwa na nidhamu nzuri ya mbinu ili kuweza kukabiliana nayo. Tumejiandaa vya kutosha,” amesema Maulid.

Amesema kikosi cha Yanga Princess kimefanyiwa maboresho kwa kuongeza wachezaji kutoka klabu mbalimbali ili kuongeza ushindani na kuwa na kikosi kipana, huku akieleza kuwa baadhi ya wachezaji wapya wanahitaji muda wa kuzoea mfumo wa timu.

Ameongeza kuwa hana hofu kuhusu ushindani wa msimu huu, akibainisha kuwa benchi la ufundi limewaandaa wachezaji kisaikolojia na linaamini kila mchezaji atakayepata nafasi atapambana kwa ajili ya ushindi.

Kwa upande wake, kocha wa JKT Queens, Kessy Juma i, amesema kikosi chake kimejiandaa vizuri kukabiliana na Yanga Princess, akisisitiza kuwa pamoja na ubora wa wapinzani wao, anaamini maandalizi ndiyo yatakayoamua matokeo ya mchezo huo.

Amesema Yanga ni timu bora na yenye ushindani, akieleza kuwa takwimu za pointi na mabao zinaonesha tofauti ndogo kati ya timu hizo, hivyo hawatarajii mchezo rahisi.

“Yanga ni timu nzuri na sisi tunajua hilo. Wao wana pointi sita na mabao matano, sisi tuna mabao manne. Ni timu bora na tumejiandaa kukutana nao,” amesema.

Related Articles

Back to top button