Kwingineko

Deschamps aitosa Manchester United

MANCHESTER: KOCHA Didier Deschamps ameiambia Manchester United kuwa hana nia ya kuwa meneja wao mpya.

Inafahamika kuwa mabosi wa United waliwasiliana na kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa kuhusu uwezekano wa kuchukua nafasi ya Michael Carrick huko Old Trafford.

Deschamps anaonekana kuwa na sifa za ushindi na uzoefu unaohitajika kukabiliana na changamoto ya kuirejesha United katika ubora wake wa zamani.

Lakini pia, alikuwa chaguo la kuvutia kwa United kwa sababu anapatikana bila gharama yoyote.

Hata hivyo, Deschamps, ambaye aliiongoza Ufaransa kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2018, hana hamu ya kujitwika jukumu hilo gumu na lenye changamoto kubwa la kuinoa United.

Deschamps alijiuzulu nafasi yake kama meneja wa Ufaransa baada ya Kombe la Dunia la majira ya joto, na kwa sasa anachukua mapumziko kabla ya kutathmini hatua yake inayofuata.

Gwiji huyo, 58 hajafanya kazi kama meneja wa klabu tangu alipoondoka Marseille mwaka 2012, na ataendelea kupima chaguzi zake kabla ya kukubali jukumu lake lijalo.

United pia ina nia ya kumteua Mhispania, Unai Emery, ambaye Jumapili hii ataiongoza Aston Villa katika mchezo dhidi ya United huko Old Trafford, inasemekana yuko karibu kukubaliana mkataba mpya na ulioboreshwa ili kusalia Villa Park.

Julian Nagelsmann pia amekuwa kwenye orodha ya wanaofuatiliwa na United, lakini hana hamu kubwa ya kufanya mazungumzo na klabu hiyo kubwa ambayo kwa sasa inapitia kipindi kigumu.

Wakati huo huo, Eddie Howe anaonekana kuwa mgombea mkuu wa kuchukua nafasi ya Carrick iwapo atafukuzwa kazi wakati wa mapumziko ya mechi za kimataifa.

Wengi walitarajia Carrick angeondolewa kabla ya mapumziko hayo ya wiki mbili, hasa ikizingatiwa kuwa United imepitia mfululizo wa mechi tisa katika mashindano yote bila kupata ushindi.

Japokuwa ushindi wa juzi wa UEFA wa mabao 3-2 dhidi ya AS Roma, umempa ahueni Carrick lakini bado hali ni tete.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button