Mastaa

Billnass: Sijawahi kuona Nandy akibadilisha shepu kwa upasuaji

DAR ES SALAAM: MUME wa msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Faustina Mfinanga ‘Nandy’, William Lyimo ‘Billnass’, amekanusha madai kuwa mkewe amewahi kufanyiwa upasuaji wa urembo (Plastic Surgery) kwa lengo la kuboresha au kuchonga shepu yake.

Billnass ameeleza kuwa tangu alipokutana na Nandy na kuvutiwa naye, hajawahi kuona mabadiliko yoyote katika mwonekano wa mwili wake, akisisitiza kuwa amekuwa akimuona akiwa vilevile tangu siku ya kwanza.

Akizungumza katika hafla ya kusherehekea albamu mpya ya Nandy, 911, Billnass alisema anampenda mkewe kwa alivyo na hajawahi kushuhudia mabadiliko ambayo yanaweza kumfanya aamini kuwa amefanyiwa upasuaji wa urembo.

“Kwa namna ambavyo nampenda mke wangu, sijawahi kuona mabadiliko yoyote katika mwili wake,” alisema Billnass.

Aliongeza: “Tangu siku ya kwanza namuona na kumtamani, kila siku namuona hivyo hivyo, na Mungu aendelee kumuweka hivyo hivyo.”

Kauli hiyo ya Billnass imekuja wakati mwonekano wa wasanii wa kike na matumizi ya taratibu mbalimbali za urembo yakiendelea kuwa miongoni mwa mada zinazozungumziwa katika tasnia ya burudani.

Nandy na Billnass wamekuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa zaidi ya miaka 10, kabla ya kufunga ndoa Julai 2022, huku wawili hao wakiendelea kuwa miongoni mwa wanandoa wanaofuatiliwa katika tasnia ya muziki nchini.

Related Articles

Back to top button