Michezo Mingine

Tanvi Patri kukutana na Zhang Yi Xin fainali ya michezo ya Olympic kwa vijana

DAKAR: MCHEZAJI chipukizi wa badminton kutoka India, Tanvi Patri, anatarajiwa kukutana na bingwa wa dunia wa vijana, Zhang Yi Xin wa China, katika fainali ya Michezo ya Olympic kwa Vijana.

Patri mwenye umri wa miaka 15 alitinga fainali baada ya kumshinda Yuzuno Watanabe wa Japan kwa seti 2-1 (21-14, 11-21, 21-19) katika mchezo wa nusu fainali.

Mchezaji huyo ana uzoefu wa mafunzo nchini China, ambako alijifunza badminton kwa miaka mitatu katika jimbo la Jiangsu chini ya makocha mbalimbali.

Patri anakuwa mwanamke wa kwanza kutoka India kufika fainali ya badminton ya mtu mmoja mmoja katika mashindano hayo, akilenga pia kuwa Mwindi wa kwanza kutwaa taji hilo.

Mwaka huu alitwaa ubingwa wa mashindano ya Asia kwa vijana chini ya miaka 17 nchini China, baada ya kuwashinda wachezaji watatu wa China katika hatua mbalimbali.

Pia amefanya vizuri katika mashindano ya kimataifa nchini Indonesia na Singapore, ambako alitwaa ubingwa na kumaliza mshindi wa pili mtawalia.

Patri amesema anajivunia kuiwakilisha India na anaamini uzoefu wake wa mashindano pamoja na maandalizi ya kimwili na kiakili utamsaidia kupambana kutwaa medali ya dhahabu.

Related Articles

Back to top button