Masumbwi

Ibrahim Class kupigana kwa ajili ya yatima

DAR ES SALAAM: BONDIA wa Tanzania, Ibrahim Class, amewataka Watanzania kujitokeza kumuunga mkono katika pambano lake la kimataifa litakalofanyika Novemba 13, mwaka huu, akisema sehemu ya mapato itatumika kusaidia watoto yatima.

Akizungumza na waandishi wa Habari Dar es Salaam leo Class amesema maandalizi ya pambano hilo yanaendelea vizuri huku akieleza kuwa wamejipanga kuhakikisha tukio hilo linafanyika kwa mafanikio, likiwa na lengo la kuunganisha michezo na shughuli za kijamii.

Amesema pambano hilo litakuwa na nafasi ya Watanzania kuchangia ustawi wa watoto yatima kupitia ununuzi wa tiketi, ambapo asilimia 20 ya mapato ya kila tiketi yataelekezwa kwa watoto hao.

“Maandalizi mpaka sasa yanaendelea vizuri. Tumejipanga na tunafanya kazi kwa ushirikiano. Tunaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kununua tiketi ili tuweze kuchangia watoto yatima,” amesema Class.

Class amesema anaamini Watanzania wana moyo wa kujitolea na wanaweza kutumia fursa hiyo kuunga mkono Watoto hao, huku akiwataka wadau wa michezo na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi.

Miongoni mwa wadhamini wa Class Meneja Mkuu wa Golden Tulip Dar City Center, Suheil Kassim amesema ana imani kubwa na bondia Ibrahim Class katika kutetea ubingwa wake, huku ikieleza dhamira yake ya kuendelea kuunga mkono maendeleo ya michezo nchini.

Amesema taasisi hiyo yenye hadhi ya nyota nne inatambua umuhimu wa michezo katika maendeleo ya Tanzania, hivyo imeamua kuungana na wadau wengine kuunga mkono pambano la Class.

Amesema kama wawekezaji nchini, wanaamini michezo ina mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla, hivyo wako tayari kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuendeleza sekta hiyo.

Related Articles

Back to top button